Tanzania yatajwa usiri wa fedha kimataifa

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Tax Justice Network Africa, Jason Braganza

Muktasari:

  • Utafiti uliofanywa na FSI umeitaja pia nchi ya Kenya ambayo imeongoza kwa nchi za Afrika Mashariki kwa kupata asilimia 80.

Dar es Salaam. Tanzania imetajwa kupata asilimia 73 ya kiwango cha usiri wa fedha (FSI) ikiwa ni miongoni mwa nchi 112 zilizopimwa duniani kote.

Utafiti uliofanywa na FSI umeitaja pia nchi ya Kenya ambayo imeongoza kwa nchi za Afrika Mashariki kwa kupata asilimia 80.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Policy Forum Dar es Salaam jana, Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Tax Justice Network Africa, Jason Braganza alisema kati ya nchi hizo, Tanzania imeshika nafasi ya 75.

“Serikali imeendelea na msimamo wake wa kuweka siri hadi itakapopelekewa hatua kamili ya maandishi ya uombwaji wa taarifa hizo,” alisema Braganza.

Alifafanua kuwa licha ya sheria za Tanzania kuvutia wawekezaji, hivi karibuni imeonekana kuwa kivutio cha usiri.

“Pamoja na kwamba sheria zipo, kuna udhaifu katika utekelezaji wa uhakiki unaofanywa na benki unaopaswa kuzingatia haki na usahihi,” alisema.

Alitaja vigezo vilivyotumika kupima usiri huo kuwa ni pamoja usajili wa umiliki usiri wa benki (asilimia 100), usajili wa taasisi (asilimia 50), rekodi ya umiliki wa kampuni asilimia 100, umiliki mwingine wa utajiri asilimia 50, uwazi wa dunia katika biashara asilimia 0.

Vingine ni uwazi wa kisheria ikiwa ni pamoja na umiliki wa kampuni za umma asilimia 100, akaunti za kampuni za umma (100), utoaji wa ripoti wa nchi kwa nchi (100), uwekaji wazi wa kodi ya shirika (100) na utambulisho wa vyombo vya sheria asilimia 100.

Katika viwango vya kimataifa, suala la uzuiaji wa utoroshaji wa fedha umepata asilimia 87, ubadilishaji wa taarifa (100), mikataba ya kikanda (100) na ushirikiano wa kisheria kimataifa asilimia 49.

Meneja msaidizi wa kodi za kimataifa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aliyekuwapo katika mkutano huo, Kayoboyo Majogoro alisema Serikali imekuwa ikipambana na ukwepaji wa kodi za kimataifa kwa nguvu zote.