Tanzania yatoa sababu ya kutosaini mkataba wa Afrika kuhusu demokrasia

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk Damasi Ndumbaro akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Tanzania ni miongoni mwa nchi 19 barani Afrika ambazo hazijasaini mkataba wa demokrasia, chaguzi na utawala bora, hadi sasa ni nchi 35 tu ndizo zimeridhia mkataba huo


Dodoma. Tanzania imetaja sababu za kutotia saini mkataba wa Afrika kuhusu demokrasia, chaguzi na utawala bora ikisema ni kutokana na baadhi ya vifungu kukinzana na ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Damasi Ndumbaro ameliambia Bunge hayo leo wakati akijibu swali bungeni.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Neema Mgaya alisema miaka sita iliyopita Tanzania ilishiriki nakupitisha azimio kuhusu masuala ya demokrasia, chaguzi na utawala bora na kutaka kujua hadi sasa Serikali imefikia wapi.

"Je Serikali inaweza kueleza ni kwa nini hadi leo azimio hilo halijaridhiwa na kusainiwa rasmi na Serikali ina mkakati gani kuhakikisha linaridhiwa?," alihoji Mgaya.

Akijibu, naibu waziri huyo alisema hadi sasa ni nchi 35 tu ndizo zimeridhia mkataba huo wakati nchi 19 hazijaridhia ikiwamo Tanzania.

Alisema wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika walikutana Januari 30, 2007 na kuzitaka nchi kuzingatia na kutekeleza utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu kama ilivyo katika ibara ya 3 na 4 ya mkataba.