Tanzania yaweka msimamo itifaki ya utalii Afrika Mashariki

Muktasari:

  • Waziri Kigwangalla asema msimamo unalenga kulinda masilahi ya Tanzania yenye vivutio vingi vya utalii

Arusha. Tanzania imefanikiwa kuzishawishi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutangaza vivutio vya utalii huku kila moja ikibaki na utambulisho wake.

Hoja hiyo imeridhiwa licha ya mjadala ulioibuka kwenye mkutano wa nane wa itifaki ya utalii na usimamizi wa wanyamapori.

Mkutano huo wa kisekta wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo ulifanyika Juni 23, 2018 jijini Arusha.

Kwenye hoja yake, Tanzania ilitaka kuboreshwa kifungu cha nne cha itifaki hiyo kinachozitaka nchi wanachama kutangaza eneo lote la EAC kama kituo kimoja cha utalii.

Kukazia msimamo wake, Tanzania ilikataa kusaini itifaki hiyo iliyojadiliwa kwa zaidi ya miaka saba kabla ya mapendekezo yake kuingizwa kwenye kifungu hicho kinachosema: "Kila nchi mwanachama itaitangaza jumuiya kama kituo kimoja cha utalii.”

Mvutano uliokuwapo kati ya Tanzania na wanachama wenzake ni mapendekezo ya kutaka maneno ‘huku kila nchi mwanachama ikibaki na utambulisho wake halisi’ yaongezwe kwenye kifungu hicho.

Katika mjadala huo, Tanzania iliungwa mkono na Burundi ikipingwa na Kenya, Uganda na Rwanda zilizosema hakuna haja ya kubadilisha kifungu hicho. Sudan Kusini haikushiriki mkutano huo.

Kutokana na mjadala, mkutano huo  ulimalizika saa nne usiku badala ya saa 12:00 jioni kulingana na ratiba.

Wajumbe walikubali mapendekezo ya Tanzania na hatimaye itifaki hiyo ikasainiwa.

Awali, itifaki hiyo ilijadiliwa na makatibu wakuu kwa siku tatu kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dk Hamisi Kigwangalla alisema: “Tanzania ililazimika kuweka msimamo huo kuepuka nchi nyingine kutangaza vivutio vyake jambo litakalopunguza watalii wanaokuja nchini.”

Alisema msimamo huo pia ulilenga kulinda masilahi ya Tanzania yenye vivutio vingi ikiwa imehifadhi ardhi yake kwa zaidi ya asilimia 32 ikilinganishwa na wanachama wengine.