Tanzanite ya Sh7.4 bil yapigwa mnada

Muktasari:

Katika mnada huo, Kampuni ya TanzaniteOne na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ziliongoza kwa kuuza madini ya Dola 3.3 milioni (Sh7.3 bilioni), huku Serikali ikiweka kibindoni mrabaha wa Sh367 milioni.

Arusha. Madini ya Tanzanite yenye thamani ya Dola 3.4 milioni za Marekani (Sh7.4 bilioni), yameuzwa kwenye mnada uliofanyika kwa siku nne jijini Arusha, huku Serikali ikipata mrabaha wa Sh378 milioni.

Katika mnada huo, Kampuni ya TanzaniteOne na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ziliongoza kwa kuuza madini ya Dola 3.3 milioni (Sh7.3 bilioni), huku Serikali ikiweka kibindoni mrabaha wa Sh367 milioni.

Katika mauzo mengine, Kampuni ya Franone iliuza madini ya Dola 100,000 (Sh215 milioni) na Serikali ilipata mrahaba wa zaidi ya Sh10 milioni.

Mkurugenzi wa Uthaminishaji Madini ya Almasi na Vito Wizara ya Nishati na Madini, Archard Karugendo amesema  hayo  Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera akifunga mnada wa Tanzanite.

Karugendo amesema wachimbaji na wanunuzi walioshiriki mnada huo ni kampuni 37, wachimbaji watano waliojitokeza ni TanzaniteOne na Stamico, Tanzanite Africa/J.S Magezi, Chusa Mining, Kurian Laizer na Franone Gems.

Amesema kampuni zinazonunua na kuuza madini ndani na nje ya nchi zilishiriki mnada huo, lengo likiwa ni kuhakikisha bei ya Tanzanite ambayo ilikuwa imeshuka inapanda na kuweka ushindani kwa njia ya minada.

Bendera amesema Tanzanite inapatikana eneo moja la Mirerani wilayani Simanjiro, hivyo Serikali itaendelea kudumisha ulinzi na usalama kwa wachimbaji.

Amesema kwa mnada huo, bei ya Tanzanite itauzwa bei inavyostahili na Wilaya ya Simanjiro itakusanya mapato yake ya kodi ya huduma kwa urahisi zaidi, hivyo kutoa huduma za jamii kwa ufanisi.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe amesema kupitia mnada huo mapato ya nchi yataongezeka hasa kwa madini ya Tanzanite, kwani mnada unafanyika eneo moja.

Profesa Mdoe amesema kwa sababu mnada huo ni wa kwanza, zipo changamoto zilizojitokeza kwani  maandalizi yamekuwa ya muda mfupi. “Kwa njia hii ya mnada huu tunakabiliana na suala la utoroshaji Tanzanite kwenda nchi za jirani, kwani wanunuzi watapata fursa ya kufika kununua wenyewe,” amesema Profesa Mdoe.