Tawa yawaondoa hofu wahifadhi juu ya mradi wa umeme wa Stiglers Gorge

Mkurugenzi Mkuu wa TAWA, Dk James Wakibara

Arusha. Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) imewaondoa hofu wahifadhi ndani ya nje ya nchi juu ya mradi wa umeme wa Stiglers Gorge ambao utatekelezwa katika eneo la pori la akiba la selous  na kueleza mradi huo utakuwa na faida kwa taifa  na uhifadhi hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TAWA, Dk James Wakibara akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 24,2018 amesema mradi huo utaleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa Tanzania wakati uzalishaji wa umeme ukianza.

Amesema sambamba na kuongeza uzalishaji wa umeme, kupitia maporomoko ya maji ya mto Rufiji katika eneo hilo la mradi ndani ya pori la akiba la Selous kutajengwa bwawa kubwa ambalo litakuwa na manufaa katika uhifadhi na utalii.

"Katika hilo bwawa tunatarajia litavutia wanyama wengi kwenda kunywa maji mwaka mzima lakini pia, tunatarajia tutaanzisha utalii maji katika eneo hilo" amesema

Amesema mradi huo, sio mgeni kwani andiko lake lilikuwepo katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) tangu mwaka 1982 kabla ya eneo hilo kutangazwa ni la urithi wa dunia.

"Tayari tathimini ya mazingira imefanyika na imefikishwa Unesco na kuonyesha mradi huo unaweza kuendelea bila kuwepo athari za kimazingira" amesema

Awali, Mwenyekiti wa bodi ya TAWA, Meja Generali mstaafu, Hamis Semfuko amesema mamlaka hiyo, itaendelea kuboresha na jitihada za uhifadhi katika maeneo ya urithi wa duniani ikiwepo selous.

Meja Generali mstaafu Semfuko ambaye bodi yake imemaliza muda wake ,alisema katika eneo la selous na maeneo mengine yaliyochini ya TAWA vitendo vyote vya ujangili vimedhibitiwa lakini pia kuna ongezeko kubwa la wanyama hasa Tembo  tofauti ya miaka ya karibuni.

Katika  eneo hilo la pori la akiba la Selous mradi mkubwa wa  umeme wa Megawati 2100 unatarajiwa kujengwa na hivyo kuondoa tatizo la umeme nchini