Taxify yatua Dodoma, Total yawapunguzia bei madereva

Muktasari:

Kampuni ya Taxify yenye makao makuu nchini Estonia inayoshindana na Uber ya Marekani imeanza kutoa huduma zake jijini Dodoma. Kampuni hiyo huwaunganisha abiria wa teksi na gari lililo jirani.

Dodoma. Dodoma limekuwa jiji la tatu kuanza kutumia huduma za Taxify, kampuni inayomuunganisha msafiri na teksi iliyo jirani yake kuanzia leo, Septemba 25, 2018.

Kwa muda mrefu, Taxify ilikuwa inatoa huduma zake jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Mwanza na sasa Dodoma.

Meneja mkuu wa Taxify nchini, Remmy Eseka anasema wanaendelea kupanua wigo wa huduma na kutokana na shughuli kuongezeka jijini Dodoma wameona wafikishe huduma zao pia.

“Huduma zetu ni salama na za bei nafuu kwa abiria kupata usafari. Tunazo ofa tofauti kwa wateja wetu wapya jijin hapa,” amesema Eseka.

Kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa uhakika, Taxify imegawa simu za kisasa (smartphone) kwa baadhi ya madereva wenye sifa lakini wenye simu za kawaida ili wapatikane watakapotafutwa na abiria walio jirani.

Madereva hao watatakiwa kulipia simu hizo kadri wanavyopata faida kwa kutumia App ya kampuni hiyo yenye makao makuu yake nchini Estonia, barani Ulaya.

Meneja mkuu wa Taxify kwa nchi za Afrika Mashariki, Shivachi Muleji amesema kila wakati wanapenda kuona mchango wao unawanufaisha wananchi wengi zaidi kwenye jamii.

"Tunafurahia kuwa wa kwanza kutoa huduma ya teknolojia ya teksi jijini Dodoma na kuwaunganisha madereva na huduma yetu. Tuna uhakika tutapunguza ucheleshewaji  kwa abiria wanaotaka usafiri kwenda sehemu tofauti za jijini hapa,” amesema Muleji.

Licha ya kuwawezesha madereva kwa simu za kisasa, Taxify imeingia mkataba wa ushirikiano na kampuni ya mafuta ya Total utakaowaruhusu madereva hao kupata mafuta kwa bei nafuu wakati wowote wanapohitaji kununua nishati hiyo.

"Daima tunatafuta fursa ambazo zitawezesha madereva kupata faida kubwa zaidi kwa kupunguza gharama za uendeshaji. Tunaamini  watafurahia kazi yao na kutoa huduma bora kwa wasafirii," amesema Eseka.