Tehama kutambua taarifa za makazi

Muktasari:

Katibu Mkuu Tamisemi, Mussa Iyombe alisema jana kuwa mfumo huo wa uingizaji wa taarifa za makazi na wakazi kwa njia ya kielektroniki unalenga kutumia teknolojia ya kisasa ili kupunguza gharama katika shughuli zake.

Dar es Salaam. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), wameanzisha mfumo wa rejesta ya makazi kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Katibu Mkuu Tamisemi, Mussa Iyombe alisema jana kuwa mfumo huo wa uingizaji wa taarifa za makazi na wakazi kwa njia ya kielektroniki unalenga kutumia teknolojia ya kisasa ili kupunguza gharama katika shughuli zake. 

“Mfumo huu utakaogharimu Sh3 bilioni utasaidia Serikali kuwatambua wavamizi na uwapo wa taarifa ya wakazi wake. Tayari tumejaribu katika Kata ya Mapinga,” alisema Iyombe.

Pia, alisema mfumo huo utasaidia kupatikana kwa idadi kamili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, walimu na kiwango cha fedha kinachotakiwa kutolewa kama ruzuku.

Alisema sehemu kubwa ya fedha hizo itatumika kutoa elimu kwa watendaji wa kata, vijiji na vitongoji kwa muda wa mwezi mmoja.

Alisema baada ya miezi mitatu kutakuwa kukifanyika tathimini kubaini changamoto na mafanikio yaliyopatikana.

Akizungumzia mfumo huo, Diwani wa Mapinga, Ibrahimu Mbonde alisema mfumo huo ni mzuri kwani utaleta takwimu sahihi tofauti na awali.

“Mfumo huu unarahisisha kazi kwani hata kwa simu unaweza kupata taarifa za mtu, vile vile unaondoa utoaji wa taarifa za uongo na kupunguza gharama ya kununua vitabu kwani kitabu kimoja kilikuwa na uwezo wa kusajili kaya 50 pekee,” alisema Mbonde.

Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Amina Said alisema mfumo huo huenda ukafuta utaratibu wa sensa ambayo imekuwa ikigharimu fedha nyingi.

Alisema fedha hizo zitatumika katika matumizi mengine kwani takwimu muhimu kuhusu watu na makazi zitakuwa tayari zipo kwenye taarifa.