Thursday, April 21, 2016

Teknolojia ya Moovn Satelaiti yanufaisha madereva 8600 Dar

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi hjumanne@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zaidi wa madereva 8600 wa vyombo vya moto katika jiji la Dar es Salaam watanufaika na huduma mpya ya kusafirisha abiria kupitia mradi wa teknolojia mpya Moovn Satelaiti.

Lengo la kuanzishwa kwa huduma hiyo ni kupunguza uhalifu unaotokana na madereva wachache wasiowaaminifu wanaotumia vyombo vya moto.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Moovn, Godwin Ndugulile amesema mradi huo wa Moovn umetengeneza teknolojia ambayo itaboresha huduma za usafiri na kuongeza usalama kwa wateja kupitia simu za mkononi za kisasa.

“Huduma hii inapatika kwa njia ya mobile application ambazo ni google Adroid na Apple ios na kwamba abiria anapohitaji usafiri wa kukodi sehemu yoyote jiji hapa, anaingia katika application hiyo na kuonana na dereva ambaye atamjibu na kisha ataenda kumchukua sehemu alipo kupitia satelite ambayo itakuwa inawaonyesha wote wawili picha zao na sehemu alipo baina ya abiria na dereva" amesema Ndugulile

Amesema kampuni yake imewekeza kiasi cha Sh2.2 bilioni kwa ajili ya huduma hiyo katika jiji la  Dar es Salaam na mradi huo umeanza kutumika tangu Machi 16,mwaka huu.

“ Lengo la kampuni ya Moovn ni kupunguza uhalifu unaotokana na madereva wachache wasiokuwa waaminifu wanaotumia vyombo vya moto” amesema Ndugulile

“Mpaka sasa tumefanikiwa kusajili madereva 8600 wa taksi, bajaji, Pikipiki katika jiji hili na kwamba kila siku tunasajili madereva kati ya 60 hadi 70 kwa siku” amesema

Ndugulile amesema kupitia huduma hiyo, madereva watatakiwa kuwa na leseni, kusajiliwa, kupata mafunzo ya usalama barabarani na kufutata sheria za zilizopo na kwamba tayari wameshakutana na Sumatra kabla ya kuanzisha huduma hiyo.

“Kampuni ya Moovn itapata faida ya asilimia 10 hadi 15 kwa kila safari moja ya dereva ambaye amejisajili kwetu” ameongeza

Meneja Mwandamizi na Uendeshaji wa kampuni hiyo, Ibrahim Ligonja amesema  teknolojia hiyo  itarahisisha  zaidi huduma ya usafirishaji wa kukodi kwa wananchi wa jiji hilo na bei za huduma hiyo zitakuwa za kamwaida kama zilivyo bei nyingine.

“Kampuni yetu ilianza kutoa huduma hii miaka miwili iliyopita katika nchi ya Marekani na kutokana na maendeleo yaliyopatikana tuliona kuna haja ya huduma hii kuianzisha nchini kwa sababu ni salama kwa abiria na mali zake” amesema Ligonja.

Kwa upande wake dereva taksi kutoka kituo cha Namanga, Elias Tupa amesema huduma hiyo ni nzuri na itaboresha kipato cha madereva wengi kwa sababu abiria watakuwa na uhuru wa kuchagua dereva ambaye yupo karibu na eneo la taksi.

 

-->