Teknolojia ya kisasa ya kupunguza taka kuanza kazi nchini

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Magdalena Mtenza

Muktasari:

Bado Tanzania haina teknolojia ya kisasa ya kuteketeza taka zinazozalishwa zaidi ya kuzichoma na hivyo kuzalisha kemikali hatari kwa mazingira ambazo zinazodaiwa kudumu kwa muda mrefu.

 

Dar es Salaam. Ofisi ya Makamu wa Rais imetambulisha mradi wa kupunguza taka kwa kutumia teknolojia ya kisasa (Upops) badala ya njia ya zamani ya kuchoma inayodaiwa kuwa na athari kubwa za kimazingira.

Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo leo Jumatatu Oktoba 15, 2018 Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Magdalena Mtenza amesema uchomaji wa taka unasababisha kuzaliwa kwa kemikali hatari kwa mazingira ambazo hudumu kwa muda mrefu.

Mtenza amesema kuwa awali mradi huo utaanza kutekelezwa katika wilaya za Ubungo na Kigamboni.

“Tunaka kuhamasisha ukusanyaji wa taka bila kuchoma, nia yetu hasa ni kuendelea kutunza mazingira,” amesema.

Awali, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uendelezaji viwanda (Unido) Dk Stephen Kagbo amesema uchafuzi wa mazingira bado ni tatizo kubwa linalozikabili nchi nyingi duniani ikiwamo Afrika.

Amesema ujio wa teknolojia ya kisasa ya kuteketeza taka hizo utasaidia utunzaji wa mazingira katika miji mingi ya nchi za Sadc

“Sadc tupo tayari kushirikiana na Tanzania katika kusaidia na mradi huu unatekelezwa katika nchi nyingine ikiwemo Botswana, Lesotho, Zambia na Madagasca,” anasema.