Telack amwapisha Macha, ampa neno
Muktasari:
Uteuzi wa Macha ulifanyika Jumapili mchana baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Fadhili Nkurlu.
Kahama. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amemwapisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamlingi Macha kisha kumtahadharisha kuwa wilaya hiyo siyo ya kuingia kizembe bali inahitaji mikakati.
“Kahama kuna changamoto nyingi ambazo ili ufanikiwe lazima uwe kamanda aliekamilika,” amemueleza Telack.
Pia amemshauri kuwa na ushirikiano na viongozi wenzake bila kuwa na uamuzi wa pekee na aitumie vizuri kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
Baada ya kuapishwa katika makao makuu ya wilaya hiyo leo Julai 17, pia Telack alimtaka Macha kuhakikisha anatekeleza maagizo ya Rais John Magufuli kuwapelekea maendeleo wananchi wa wilaya hiyo.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Thomas Muyomba amemtaka Macha kusimamia vizuri utekelezaji wa ilani ya CCM na kuahidi kumpatia ushirikiano kila patakaohitajika kufanya hivyo.
“Wananchi wa Kahama ni wasikivu hivyo wana imani nawe kama ulivyoaminiwa na Rais Magufuli kuja kufanya kazi hapa,” amesema
Hata hivyo, Macha hakuweza kusema lolote na atazungumza wakati mwingine pindi atakapopata muda mwingine wa kuzungumza na kutoa mikakati yake.
Uteuzi wa Macha ulifanyika Jumapili mchana baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Fadhili Nkurlu wakati akiwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye jana alimaliza ziara yake ya siku nne wilayani hapo.