Temesa yanunua boti nne

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Dk Mussa Mgwatu

Muktasari:

  • Akiwa katika karakana ya kampuni hiyo jana, Dk Mgwatu alisema Serikali imepanga kutekeleza mradi huo ili kutoa huduma za usafiri wa majini kwa wananchi kwenye maeneo manne tofauti.

Mwanza. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Dk Mussa Mgwatu ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa boti nne za kisasa unaotekelezwa na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard jijini Mwanza.

Akiwa katika karakana ya kampuni hiyo jana, Dk Mgwatu alisema Serikali imepanga kutekeleza mradi huo ili kutoa huduma za usafiri wa majini kwa wananchi kwenye maeneo manne tofauti.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Pangani mkoani Tanga ambako wananchi walimuomba Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akizindua Kivuko cha Mv Tanga kuwapelekea boti ndogo itakayowasaidia katika kazi za dharura nyakati za usiku.

Dk Mgwatu alisema boti ya pili itapelekwa Msangamkuu mkoani Mtwara nako vilevile itakuwa inatumika kwa kazi za dharura. Boti hizo mbili zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria wanane kila moja.

Boti ya tatu inatarajiwa kupelekwa Kilambo, mkoani Mtwara ambako Kivuko cha Mv Kilambo kinatoa huduma ya kuvusha wananchi kati ya upande wa Tanzania na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma.

Alisema boti hiyo itatumika katika vipindi ambavyo maji yanapopungua kwenye mto huo, ili kuvuta Kivuko cha Mv Kilambo na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 25.

Boti ya nne itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 40 na itapelekwa eneo la Utete mkoani Pwani, ili kutoa huduma wakati wote hata maji ya Mto Rufiji yanapopungua.

Mhandisi wa Kampuni ya Songoro Marine Boatyard, Major Songoro alisema kazi ya kujenga boti zote inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.