Tendaguru; kivutio cha mijusi ya zamani kilichotelekezwa

Muktasari:

  • Mijusi hao aina ya dinosaria walitoweka baada ya kushindwa kuhimili mazingira mapya na ushahidi kuwa viumbe hao waliishi Tanzania upo katika kilima hiki.

Kilima cha Tendaguru kilichopo kwenye msitu wa kijiji cha Mnyangala wilaya ya Lindi Vijijini, ndiyo makazi ya asili ya mijusi wakubwa waliotoweka duniani.

Mijusi hao aina ya dinosaria walitoweka baada ya kushindwa kuhimili mazingira mapya na ushahidi kuwa viumbe hao waliishi Tanzania upo katika kilima hiki.

Hakuna miundombinu ya barabara ya kuelekea katika eneo hili la kihistoria. Unahitaji muda wa zaidi ya saa moja kwa usafiri wa pikipiki ukikatisha kwenye msitu.

Dinosaria ni nini?

Watafiti wanasema ni viumbe wakubwa walioishi duniani zaidi ya miaka 200 milioni na kilima cha Tendaguru, ni miongoni mwa maeneo yanayotumika kama rejea ya uwepo wa viumbe hivyo kwenye uso wa dunia.

Mwaka 1842 familia ya viumbe hao ilipewa jina la ‘dinosaur’ na mtafiti Richard Owen ikiwa ni lugha ya Kigiriki ikimaanisha mijusi wa kutisha.

Juu ya kilima hiki kati ya mwaka 1909 na 1913 yalichimbuliwa mabaki ya kiumbe hicho na kusafirishwa hadi nchini Ujerumani na kuhifadhiwa kwenye jumba la makumbusho.

Maajabu juu ya kilima

Kuna njia fupi ya kuelekea juu ya kilima kwa kufuata miti iliyowekewa alama ambayo inakuongoza hadi kwenye kilele yalipochukuliwa mabaki ya dinosaria.

Kuna eneo la hatua 37 (kadri nilivyohesabu) ambalo limezungushiwa mawe ya mviringo mfano wa ramani ya mnyama na kuwa hapo ndipo yalipochimbwa mabaki ya kiumbe hicho.

Hakuna maelezo katika eneo hili yanayotaja sababu za kiumbe hicho kuchagua kufia juu ya kilima na historia ya kivutio hiki, inahifadhiwa kupitia simulizi za wazee kwa wajukuu wao.

Mashimo juu ya kilima

Simulizi za kugundulika kwa mabaki hayo zimevutia wananchi kuamini kuwa kwenye kilima hicho, kuna vitu vya thamani na kuwa sababu ya kuwepo kwa mashimo mengi.

Mkazi wa kijiji cha Mkwajuni kata ya Kitomanga, Masoud Faragha anasema alipata vipande viwili mfano wa mifupa na kuviuza kwa mgeni kutoka Ujerumani.

‘’Ni kama mjusi alikuwepo kweli nilichimba na kupata vipande viwili vya mifupa niliviuza kwa Sh 200,000 kwa raia wa Ujerumani aliyekuwa anaishi Mtwara,’’ anasema Faragha.

Inaendelea Uk 26

Inatoka Uk 25

Hakuna utaratibu maalumu wa kusimamia na kuhifadhi eneo hili lililozungukwa na misitu ambayo ni makazi ya wanyama kama tembo, nyati, swala, ngiri na aina tofauti za ndege.

Sheria namba 10 ya mwaka 1964 na marekebisho ya mwaka 1979 inampa mamlaka mkurugenzi wa malikale na waziri kutangaza eneo lihifadhiwe kama linafaa kwa mujibu wa sheria.

Tofauti ya Tendaguru na Tendeguru

Wenyeji wa kijiji cha Mnyangala kata ya Mipingo wanakitaja kilima hiki kwa jina ya Tendeguru na si Tendaguru kama ilivyonukuliwa katika maandiko mbalimbali.

Mzee Rashid Nkape (81) anasema kilima kilitumika kwa ajili ya matambiko na kuwa Wazungu walishindwa kutamka kwa usahihi jina la Mzee Tendeguru aliyeishi karibu na kilima hicho na badala yake kutamka Tendaguru.

Kosa la usahihi wa maneno pia linaonekana katika chimbuko la historia ya zamadamu katika Bonde la Oldupai ambapo mtafiti Profesa Wilhalm Windle alishindwa kulinukuu vema na kuandika Olduvai.

Kwa mujibu wa mhifadhi wa mali kale wa bonde hilo John Paresso, Oldupai ni lugha ya Kimasai unapotajwa mmea wa katani unaopatikana kwenye eneo hilo.

Wageni kilimani

Umuhimu wa kilima cha Tendaguru pia umevutia wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani hususani nchini Ujerumani na hakuna mwenye uhakika kama wanafika kama watalii au watafiti.

Mwenyekiti wa kijiji Bakari Meno anasema wanapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi wanaoelekea kilima cha Tendaguru na hakuna mapato yanayobaki.

Ofisa maliasili Mkoa wa Lindi, Zawadi Jilala anasema hakuna mfumo wa kuratibu na kusajili wageni wanaofika katika kijiji hicho kutembelea kilima cha Tendaguru.

Anasema eneo hilo halijatangazwa wala kuendelezwa hivyo hakuna mapato yanayovunwa na kuwa idadi kubwa ya wageni wanaovutiwa kulitembelea ni kutoka nchini Ujerumani.

‘’Inawezekana kuna ukweli haujafahamika kuhusu mifupa iliyochukuliwa Tendaguru, wageni wengi wanaofika kutembelea eneo hilo ni kutoka Ujerumani,’’anasema Jilala.

Anataja changamoto kubwa ya kuelekea eneo hilo ni kutofikiwa kwa urahisi na kuwa hata mipango ya kuboresha miundombinu ya barabara huenda ikachukua muda mrefu ujao.

Diwani wa Kata ya Mipingo, Said Naomary anasema mara kadhaa amewasilisha ajenda kwenye baraza la madiwani ili eneo hilo liboreshwe na kutumika kama chanzo cha mapato kupitia utalii lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Mtafiti wa mali kale aonya

Mtafiti na mkufunzi wa malikale wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk Elgidius Ichumbaki anasema kilima cha Tendaguru kinabeba historia na umuhimu wa pekee kuhusu mijusi waliotoweka.

Anaonya kuwa kilima hicho ni rasilimali yenye umri wa zaidi ya miaka mia moja na kwa umri huo tayari kina ulinzi kisheria na eneo muhimu kwa tafiti.

‘’Hilo ni eneo linalotakiwa kulindwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria ili hata vizazi vijavyo viendelee kujifunza hiyo mijusi haipo tena duniani na pengine kuna mabaki mengine’’anasema Dokta Ichumbaki

Anaitaka Serikali ione umuhimu wa kuwa na miundombinu ili kurejeshwa kwa mabaki ya kiumbe hicho aliyosema yananufaisha nchi nyingine kupitia shughuli za utalii.

‘‘Kwa kutorudisha mabaki tunaendelea kupoteza fedha lakini zile ni nyara za Serikali tunaonyesha uzembe katika ulinzi na utunzaji rasilimali zetu tunawapa kipato watu wengine,’’ anasema Dk Ichumbaki

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa na mkuu wa idara ya Utalii na Utamaduni, Jimson Sanga anasema ni wajibu wetu kulinda na kuhifadhi rasilimali zetu vikiwa vivutio vya utalii.

Anasema kinyume chake ni kupoteza urithi na ushahidi muhimu kwa vizazi vijavyo akitoa mfano wa kurejeshwa fuvu la chifu Mkwawa kama ushahidi unaopatikana nchini wa kiongozi wa Kiafrika aliyekataa kutawaliwa na wakoloni.

Makumbusho ya Taifa

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Profesa Audax Mabulla anasema kilima cha Tendaguru ni eneo muhimu utafiti ingawa kuna changamoto ya kufikia eneo hilo.

Kwa mujibu wa Profesa Mabulla mabaki ya kiumbe hicho baadhi huyalinganisha na ghorofa katika simulizi zao na kuwa kimo chake ni kati ya mita 13-15 na urefu kati ya mita 25-30

Anasema kuna gharama kubwa za kutunza mabaki ya dinosaria yaliyochukuliwa Tendaguru ikiwa yatarudishwa kwa kuwa nchi haijawa na wataalamu katika eneo hilo, lazima waandaliwe kwanza. ‘’Gharama za utunzaji ni kubwa kuna masuala ya kisayansi unahitaji uamuzi mzito, lazima wawepo wataalamu kila kitu kinahitaji maandalizi lakini tukiwa na nia ya dhati tunaweza,’’ anasema Profesa Mabulla.

Tendaguru ndani ya Bunge

Katika kikao cha Bunge Juni, 2017 aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Ramo Makani alilazimika kujibu maswali ya wabunge kuhusu kusahaulika kwa kivutio cha Tendaguru.

Mbunge wa Jimbo la Mchinga kilipo kivutio hicho, Hamidu Bobali alihoji mchango wa kivutio hicho na masalia yaliyosafirishwa kwenda Ujerumani katika kuboresha maisha ya wananchi wa kijiji cha Mnyangala.

Mbunge wa Tarime mjini Ester Matiko aliuliza swali la nyongeza akihoji sababu za rasilimali hiyo kuendelea kuhifadhiwa nje ya nchi na kutaka kujua kiwango cha mgao tunaopata kama taifa kupitia rasilimali hiyo iliyochukuliwa Tendaguru.

Katika majibu yake naibu waziri huyo alisema mazungumzo yanaendelea kati ya nchi hizo na wamekubaliana uboreshaji wa idara ya malikale katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam na mipango ya wananchi kunufaika na eneo hilo iko mbioni inakuja.