Tetemeko la ardhi linavyoumiza vichwa vya wanasayansi Duniani

Muktasari:

Miongoni mwa maswali wanayojiuliza ni, tetemeko la ardhi ni kitu gani? Kwanini hutokea ghafla? Kwanini hutokea zaidi baadhi ya maeneo? Na Kwanini kuna ugumu kulizuia na kulitabiri na pengine linasababishwa na nini?

Wapo wanaodadisi na kujiuliza maswali mengi kuhusu tetemeko la ardhi, bila shaka miongoni mwa watu hawa wengi wao ni wale ambao tayari wameathirika na tetemeko la ardhi.

Miongoni mwa maswali wanayojiuliza ni, tetemeko la ardhi ni kitu gani? Kwanini hutokea ghafla? Kwanini hutokea zaidi baadhi ya maeneo? Na Kwanini kuna ugumu kulizuia na kulitabiri na pengine linasababishwa na nini?

Jambo la kwanza kabisa unapaswa kutambua kwamba, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimepitiwa na ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki kwa mikondo miwili.

Upo mkondo wa Mashariki ambao unapita kwenye mikoa ya Mara, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma, Iringa, Njombe na Ruvuma wakati mkondo wa Magharibi unapita mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Mbeya.

Kuwepo kwa ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki ni muendelezo wa nguvu za asili ambazo hapo awali zilisababisha kutokea kwa mabara saba tuliyonayo sasa baada ya kugawanyika kwa bara moja la kwanza la dunia (Supercontinent).

Kwa mujibu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), mabadiliko hayo ya kijiolojia huenda yakasababisha nchi za Djibout, Ethiopia, Somalia, Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Msumbiji kujitenga na kuwa visiwa ndani ya Bahari ya Hindi.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa GST ni kwamba, maeneo ya ukanda wa Bonde la Ufa hukumbwa na matetemeko ya ardhi ya mara kwa mara kutokana na eneo hilo kuwa tete lenye fukuto kubwa la joto.

Aprili 14, 2018 kulisambaa taarifa za mshtuko katika mitandao ya kijamii inayodaiwa kutolewa na Shirika la China Global Television Network (CGTN) zinazoeleza kwamba wanasayansi wametabiri kutokea tetemeko la ardhi nchini Tanzania mwaka 2019, ikiwa ni jingne baada ya lile la mkoani Kagera.

Hata hivyo, Mjiolojia Mwanandamizi wa GST, Gabriel Mbogoni anatoa sababu za kukosekana kwa utabiri wa kutokea matetemeko.

Anasema ili kufanikisha utabiri wa aina hiyo, inatakiwa ufanyike utafiti utakaoonyesha ni wakati gani mwamba wa mahali husika utafikia kiwango ambacho utashindwa kuhimili nguvu za mgandamizo na ndipo ukatike ama usigane na tabaka jingine la mwamba.

Pili, anasema ni vigumu pia kujua hizo nguvu za mgandamizo zina msukumo wa kiasi gani, na zitaendelea kugandamiza eneo hilo kwa muda gani, kwa kuwa ni nguvu za asili na zinatokea katika kina kirefu sana cha ardhi.

“Utafiti wa aina hii ambao kuna mambo mengi yanayopaswa kuzingatiwa na kwa vile ni mengi na ambayo hayapo kwenye uwezo wa binadamu inakuwa vigumu kutafuta majawabu yake,’’ anasema Mbogoni.

“Duniani kote hakuna teknolojia ya kutabiri matetemeko ya ardhi iliyowahi kuwa ya mafanikio, hadi hivi sasa wanasayansi bado wanaendelea na jitahada hizo,” anasema.

Anasema matetemeko ya ardhi kwa kawaida husababishwa na nguvu za asili za mgandamizo ambazo husababisha kukatika ama kusigana kwa matabaka ya miamba katika kina kirefu chini ya ardhi.

Mbogoni anasema nguvu hizo hujikusanya kwa muda mrefu, wakati mwingine inaweza kuchukua hata miaka 1000 kufikia kiwango ambacho mwamba utashindwa kuhimili nguvu hizo za mgandamizo kabla ya kutikisika kwa ardhi.

Mtikisiko huo husambaa maeneo mbalimbali kwa njia ya mawimbi ambayo husafiri kwa kasi ya kati ya kilomita 8 hadi 13 kwa sekunde moja kulingana na aina ya asili ya miamba.

“Lakini pia, kutokana na nguvu za asili za mgandamizo kujikusanya kwa muda mrefu, ni vigumu kujua tabia za miamba ya eneo husika kutokana na ukubwa wake, na pengine kujua ni wapi hasa patatokea tetemeko, kwa kuwa miamba inatofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine japo inawezekana miamba hiyo ikawa ya asili moja,” anasema.

Kutokana na mazingira hayo, Mbogoni anasema hadi sasa Duniani kote wanasayansi hawajaweza kugundua namna ya kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi.

“Kwa hiyo utabiri unaotolewa kuhusu tetemeko litakalotokea Tanzania hapo mwakani ni sawa na kurusha jiwe kwenye kundi la nyuki ambapo, unajua kabisa huwezi kukosa kumpata angalau nyuki mmoja. Tanzania iko kwenye ukanda wa Bonde la Ufa ambao matetemeko ya ardhi ni jambo dhahiri kutokea,” anafafanua Mbogoni.

Japan inavyopambana

Mbogoni pia anasema tetemeko hilo halisumbui nchi maskini, hata zilizoendelea kwa teknolojia ya sayansi duniani kama Japan na China bado zinakumbwa na matetemeko ya ardhi kwa kuwa hazijagundua namna ya kutabiri matukio ya matetemeko ya ardhi. Kwa kawaida, tetemeko la ardhi husafiri kwa njia ya mawimbi ambayo husambaa pande zote kutoka kwenye chanzo. Wanasayansi wanatambua aina mbili: mawimbi yanayotangulia kwa kasi ndogo (Mawimbi P) na yale yanayosafiri kwa kasi kubwa (Mawimbi S).

Mawimbi hayo hutofautiana muda wa kuwasili, inaweza kufikia tofauti ya hadi sekunde 20. Mawimbi hayo yanaathiri maeneo kwa tofauti ya kasi ya mawimbi yenyewe.

Akitoa mfano wa juhudi za Japan anasema walichofanya wanasayansi wao ni kuweka mfumo ambao Mawimbi ya ‘P’ yanapofika kwenye mitambo ya kuratibu matetemeko ya ardhi mfumo ule unatoa taarifa (alarm) kupitia simu za mkononi. “Mwaka 2016 nilitembelea Chuo Kikuu cha Tokyo, nikakutana na Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa matetemeko ya ardhi Japan, Profesa Hiroshi Satto ambaye alisema mfumo huo bado haujawa wa manufaa, tatizo ni kwamba kwa matetemeko ambayo chanzo chake kipo karibu P na S, mawimbi yake hufika pamoja kwa hiyo wakati mtu anaposikia kengele kwenye simu yake ni wakati huo huo anatikiswa na tetemeko kwa hiyo mtu hapati nafasi ya kufanya lolote kwa ajili ya tahadhari,”anasema.

Anasema kwa milipuko ya volkano wakati mwingine inawezekana kukawa na viashiria inapopanda kwenye uso wa Dunia lakini kwa tetemeko la ardhi, hakuna ishara ya kujua litatokea lini.

Utabiri wa matukio

Hata hivyo, mjiolojia huyo anasema kwa kiasi kidogo inawezekana kutabiri kutokea tetemeko la ardhi kwa kutumia matukio ya kihistoria ya matetemeko ya ardhi yaliyowahi kutokea. Anasema mtu anapaswa kujua kutokana na historia kwamba matetemeko yanatokea katika eneo husika kila baada ya muda gani na imetokea hivyo mara ngapi.

“Njia hii hutumiwa lakini si ya uhakika, taarifa kama hii inamaanisha unaongelea tofauti ya miaka 30 kwenye utabiri wa aina hiyo,”anasema.

Tofauti Tanzania, Duniani

Tanzania iliwahi kukumbwa na tetemeko kubwa la ardhi Desemba 13, 1910 ambalo lilikuwa na ukubwa wa richa 7.4, ikiwa ni historia ya kutokea kwa tetemeko lenye ukubwa kama huo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Matetemeko mengine makubwa ni pamoja na lile lililotokea Kagera, Septemba 2016 la ukubwa wa 5.7 katika kipimo cha richa ambalo bado lipo katika kumbukumbu za wananchi wengi ambalo lilisababisha vifo vya watu 17, majeruhi zaidi ya 500, uharibifu wa nyumba 270 na miundombinu ya utoaji huduma za jamii. Matetemeko mengine ni yale yaliyotokea Arusha mwaka 2007, Mlima Oldonyo Lengai ulipokuwa ukifukuta na kulipuka, yakiwamo ya ukubwa wa richa 5.9.

China ndiyo inayoongoza kwa idadi ya vifo vya matetemeko ya ardhi, kuanzia mwaka 1900 hadi 2016, watu wapatao 876,400 walipoteza maisha ikifuatiwa na Haiti, Indonesia na Japan.

Matukio ya matetemeko ya ardhi yanaendelea kutokea kila siku nchini humo na kusababisha madhara.

“Ukweli sina hakika na utabiri wao labda ni ugunduzi mpya ambao hata hivyo tungeshafahamu kwani isingekuwa kitu cha kuficha katika ulimwengu wa sayansi, ila ninachokifahamu hadi sasa Duniani kote hakuna teknolojia ya kutabiri kutokea tetemeko la ardhi.”

Namna ya kuchukua tahadhari

GST inashauri watu kukaa mahali salama, eneo lililo wazi, lisilo na majengo marefu, miti mirefu na miinuko mikali.

Tahadhari nyingine wakati wa tukio ni kutotembea umbali mrefu kwa lengo la kutafuta mahali salama kwani takwimu zinaonyesha watu wanaotaharuki na kukimbia ovyo wakati wa tukio la tetemeko ndiyo hupata madhara.

Inashauriwa kujihadhari na matukio ya moto kwani tetemeko la ardhi linaweza kusababisha kupasuka mabomba ya gesi au kukatika kwa nyaya za umeme na kama unaendesha chombo cha moto simama kwa uangalifu sehemu salama, subiri hadi mitetemo imalizike. Pia inashauriwa kuzima umeme ili kuepuka kutokea hitilafu ya umeme kwani mitetemo huenda ikaendelea na ni muhimu kuita wataalamu wa majengo ili wayafanyie ukaguzi.