Teu asimulia alivyopata taarifa ya vifo vya ndugu yake

Muktasari:

Ndugu wa Gregory Teu walifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea nchini Uganda.

Naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, Gregory Teu ameeleza namna aliyopokea taarifa ya kufariki dunia ndugu zake 13 katika ajali iliyotokea usiku wa kuamkia jana Jumatatu nchini Uganda.

Teu alihudumu kwa nafasi hiyo katika Wizara ya Fedha na baadaye Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, akiwa mbunge wa Mpwapwa.

Akizungumza leo Jumanne jijini hapa nyumbani kwake Mtaa wa Kaunda eneo la Oysterbay amesema binti yake Dk Aneth alifanyiwa hafla ya kuagwa mwishoni mwa wiki iliyopita kabla ya kwenda Uganda kufunga ndoa Jumamosi iliyopita.

Teu amesema baada ya hafla kumalizika,  baadhi ya wanafamilia walipanda basi na walitangulia kuondoka saa 10:00 jioni kurudi Tanzania.

Amesema yeye, mkewe na baadhi ya watoto walisubiri kupanda ndege saa sita usiku na walifika Dar es Salaam saa nane  usiku.

"Tulipokewa na familia iliyobaki nyumbani, lakini badala ya furaha ilikuwa majonzi kwa kuwa wenzetu walishapata taarifa kuwa waliotangulia kwa basi wamepata ajali. Taarifa ilinishtua lakini swali likabaki ni nani na nani waliofariki kwenye ajali hiyo," amesema.

Teu amesema baada ya muda walipata taarifa kamili za waliofariki baadhi wakiwa ni baba yake mzazi na kijana wake wa kwanza, Sakazi Teu.

Amesema miili ya ndugu zake itawasili Dar es Salaam leo usiku na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo ambako itaagwa kesho asubuhi hospitalini hapo na baadaye itasafirishwa kwa maziko yatakayofanyika Mpwapwa na Kilimanjaro.

"Kama familia tumekubaliana mazishi kufanyika wilayani Mpwapwa ambako ndiko kwetu siku ya Alhamisi ambako itazikwa miili sita. Ijumaa itakuwa mazishi ya Kilimanjaro ambako ni miili saba," amesema Teu.

Amesema binti yake waliyekwenda kumuozesha Dk Aneth Teu na mumewe Dk Trease Ibingira na ndugu wanane kutoka familia ya Profesa Ibingira ambaye ni mkwewe watawasili nchini leo.

Amesema binti yake amemaliza masomo ya udaktari wa binadamu katika Chuo cha KCMC walikokutana na mumewe ambaye pia alikuwa akisoma udaktari.

Teu ameishukuru Serikali ya Uganda kwa ushirikiano waliotoa ikiwemo kukodi ndege ya kurudisha miili hiyo nchini.

Pia, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ikiwemo kukodi magari mawili kwa ajili ya kusafirisha miili hiyo na eneo la kuihifadhi katika Hospitali ya Jeshi Lugalo.