Mvua yaongeza theluji Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Shelutete amesema mvua ilinyesha Januari Mosi,2018.

Moshi. Kuongezeka theluji katika Mlima Kilimanjaro kumekuwa kivutio kwa wananchi ambao baadhi wamekuwa wakipiga picha mandhari ya mlima huo.
Hata hivyo, baadhi wamekuwa wakihoji iwapo hali itaendelea kuwa hivyo.
Akizungumzia hali hiyo, Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Paschal Shelutete amesema hali hiyo inatokana na mvua iliyonyesha Januari Mosi,2018.
Shelutete amesema leo Januari 3,2018 kuwa mvua inayonyesha kwenye uwanda wa juu kuanzia mita 3,500 kutoka usawa wa bahari inakuwa katika mfumo wa theluji.
Amesema hali hiyo inatokana na kiwango kidogo cha joto ambacho kwa usiku hufika hasi (sentigredi sifuri au chini).
“Theluji hii huyeyuka kukiwa na mabadiliko ya hali ya hewa hasa kiangazi (kunapokuwa na jua). Upande mwingine kukiwepo na mvua endelevu na mabadiliko ya hali ya jua na joto theluji huungana na kuwa barafu ya kudumu,” amesema.
Mwongozaji watalii katika kampuni ya Zara Adventures Tours ambaye pia ni mwenyekiti wa waongoza watalii katika Mlima Kilimanjaro na Meru, Faustine Chombo amesema theluji imeongezeka lakini ni ya muda kutokana na mvua iliyonyesha.
Amesema hali ya hewa katika Mlima Kilimanjaro kwa sasa ni ya mvua ndiyo maana ukiuangalia mlima kutokea Moshi mjini unaonekana kuwa na theluji nyingi.
Amesema wamejipanga kupanda miti kila mwaka katika maeneo ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ili kusaidia jitihada za kuulinda na kuuhifadhi.
Chombo amesema kuna haja ya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuhamasishwa kupanda miti kwa wingi katika maeneo ya hifadhi hiyo hatua itakayosaidia theluji kuendelea kuwapo.