Tigo kuwaunganisha abiria, madereva teksi, bodaboda

Mkuu wa Zana za Kidijitali wa Kampuni ya Simu ya Tigo, Tawonga Mpore (kushoto), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kampuni hiyo kuzindua Twende APP kwa ajili ya kusaidia huduma ya usafiri wa teksi nchini.

Muktasari:

Programu hiyo inawaunganisha madereva wa teksi, bodaboda au bajaji na kumuwezesha abiria kulipia kupitia Tigo Pesa kwa gharama za chini kuliko ambavyo angetumia njia mbadala.

Dar es Salaam. Ili kutoa suluhisho kwa changamoto za huduma za usafiri, Kampuni ya Tigo imezindua huduma mpya ya Twende App inayoweza kuita teksi iliyo jirani na wateja kote nchini.

Programu hiyo inawaunganisha madereva wa teksi, bodaboda au bajaji na kumuwezesha abiria kulipia kupitia Tigo Pesa kwa gharama za chini kuliko ambavyo angetumia njia mbadala.

Akitangaza huduma hiyo mpya, Mkuu wa zana za dijitali wa Tigo, Tawonga Mpore alisema Twende App itakuwa na mawasiliano ya madereva ambao wamehalalishwa na vyama vyao kutoka maeneo mbalimbali.

“Tunafahamu msongamano wa magari uliopo jijini kwa sasa hivyo tunalenga kuwa sehemu ya kutatua adha hiyo. Kupunguza usumbufu barabarani na athari zinazotokana na msongamano wa magari ni sehemu ya kukua kwa uchumi,” alisema Mpore.

Programu imetengezewa na Justin Kashaigili chini ya usimamizi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Hassan Mshinda aliishukuru Tigo kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia uvumbuzi nchini.

“Tigo inasaidia wajasiriamali vijana katika teknolojia kupata msaada wa kufanikisha malengo yao. Naamini, huduma hii itakuwa na ina wapatia manufaa madereva kote jijini,” alisema Dk Mshinda.

Kashaigili alisema kasi ya maendeleo ya miundombinu na ongezeko la ujasiriamali nchini ndivyo vilivyomsukuma kubuni Twende App. “Nategemea kuwapatia wananchi chaguo wanalolimudu, rahisi na linalofaa kwa ajili ya usafiri salama,” alisema.

Kujiunga na huduma hiyo, abiria anatakiwa kupakua Twende App kwenye simu yake ambayo itamuunganisha moja kwa moja na dereva kila atakapokuwa badala ya kuhangaika kutafuta sehemu ilipo teksi.

Huduma hii, pia inatumia muda sahihi wa taarifa za dereva, mfumo hai wa satelaiti unaowezesha ramani ya kufahamu sehemu alipo abiria kabla ya kumuunganisha na dereva aliye karibu na wakati huohuo kumwezesha dereva kutoa majibu kuhusu mahitaji ya mteja.

Baada ya kuunganishwa na huduma kutolewa, malipo yatafanyika kupitia Tigo Pesa kwa namba binafsi za dereva.