Tira yazifutia leseni kampuni nne

Muktasari:

Kampuni za udalali wa bima huwajibika kwenye kampuni za bima kwa kuwatafutia wateja wa bima.


Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) imezifutia leseni kampuni nne za ushauri na udalali wa bima (insurance brokers), kwa kushindwa kuwasilisha ada za wateja kwenye kampuni za bima na wamiliki wake sasa wanatafutwa na polisi.

Kampuni za udalali wa bima huwajibika kwenye kampuni za bima kwa kuwatafutia wateja wa bima.

Akizungumza leo Alhamisi Machi 22, 2018  Kamishna wa Bima, Dk Baghayo Saqware amesema kampuni hizo zilipokea ada za wateja, lakini hazikupeleka kwenye kampuni za bima na kusababisha usumbufu kwa wateja.

Zilizonyang’anywa leseni ni kampuni ya udalali wa Bima ya Hans ambayo ilishindwa kuwasilisha ada kwenye Kampuni ya Bima ya UAP.

Dk Saqware ameitaja kampuni nyingine kuwa ni Bima Endeavour ambayo ilishindwa kuwasilisha ada kwenye kampuni ya UAP na kuwasababishia wateja usumbufu.

Kampuni nyingine ni Bima Legend of East Africa ambayo ilishindwa kuwasilisha ada za wateja wake kwenye kampuni ya Bima ya MGen.

Kamishna amesema kampuni ya udalali wa Bima ya Swift yenyewe pamoja na kushindwa kuwasilisha ada za wateja, wamiliki wa kampuni wamefunga ofisi na hawajulikani walipo.

Amesema pamoja na kuzifutia leseni mamlaka inashirikiana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili kuhakikisha wamiliki wanapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Sheria wa Tira, Magreth Mngumi amesema mamlaka hiyo iko imara kuhakikisha sekta ya bima nchini inakuwa chachu ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.