Tizeba apinga taarifa za polisi ajali iliyoua watumishi watano Wizara ya Kilimo

Muktasari:

Waziri wa Kilimo Dk Charles Tizeba amepinga taarifa ya Polisi Mkoa wa Singida kuhusu ajali ya gari ya wizara hiyo iliyosababisha vifo vya wafanyakazi watano wa wizara

 


Dodoma. Waziri wa Kilimo Dk Charles Tizeba amepinga taarifa ya Polisi Mkoa wa Singida kuhusu ajali ya gari ya wizara hiyo iliyosababisha vifo vya wafanyakazi watano wa wizara.

Ajali hiyo ilitokea Jumapili Oktoba 21 mkoani Singida baada ya gari lao aina ya Mitsubishi Pajero kugongana uso kwa uso na lori.

Muda mfupi baada ya kutokea ajali hiyo zilisambaa picha katika mitandao ya kijamii zikionyesha gari hiyo kuwa katika spidi 89 katika eneo lenye kibao kinachoonyesha spidi inayotakiwa ni 50.

Akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya mazishi ya  watumishi hao leo Oktoba 23, 2018, Dk Tizeba amesema jana alitumia muda mwingi kuzungumza na wananchi na dereva wa roli lililosababisha ajari hiyo.

"Nawaomba polisi wa Singida warudie taarifa zao, wamehukumu na mitandao mbalimbali nayo imehukumu. Hili si kweli hata kidogo. Napinga taarifa zile zimejaa upotoshaji na hukumu isiyo ya kweli," amesema Tizeba.

Waziri Tizeba amesema mita chache kutoka  eneo ilipotokea ajali hiyo kuna tuta kubwa ambalo gari haliwezi kupita likiwa katika mwendo mkali.

Hata hivyo, amekiri dereva wa gari hilo alikuwa akiyapita magari mengine na kwamba lori lililogongana na gari hilo la wizara lilikuwa limeegeshwa pembeni lakini liliingia ghafla barabarani.

Watumishi hao ni Stella Joram Ossano (39), Esta Tadayo Mutatembwa (36), Abdallah Selemani Mushumbusi (53), Charles Josephat Somi na Erasto Mhina (43).