Tofauti ya UTI na STI ni hii hapa

Muktasari:

UTI ni kifupi kinachojulikana sana kwa wagonjwa hasa wanawake, kirefu chake ni Urinary Track Infections kwa kiswahili ni uambukizi wa njia ya mkojo.

Leo imenilazimu nitoe ufafanuzi kuhusu tofauti ya UTI na STI au STD, wapo baadhi ya wasomaji wanaonitumia ujumbe kuwa hawaelewi matatizo haya ya kiafya.

UTI ni kifupi kinachojulikana sana kwa wagonjwa hasa wanawake, kirefu chake ni Urinary Track Infections kwa kiswahili ni uambukizi wa njia ya mkojo.

Njia ya mkojo huanzia katika figo, mrija unaosafirisha mkojo kutoka katika figo kwenda kwenye kibofu cha mkojo (Ureter), kibofu cha mkojo na mrija wa kutolea mkojo, toka kwenye kibofu kwenda nje ya mwili (Urethra).

Wakati STD au STI kirefu chake ni Sexually Transmitted Diseases au Infections, yaani maradhi yanayoenea kwa njia ya kujamiana aidha ni kwa njia ya uke, njia ya haja kubwa au mdomo.

Ikumbukwe kuwa UTI kwa wanawake hutokea katika njia ya mkojo wakati STI hutokea ukeni na viungo vya uzazi ikiwamo mlango wa mji wa mimba, mirija ya uzazi na mji wa mimba.

Kwa mwanaume, UTI hutokea katika njia ya mkojo na STI hutokea mrija wa kutolea nje mkojo (Urethral) na viungo vya uzazi vya kiume ikiwamo uume, tezi dume, mirija ya kupitishia mbegu na kokwa za kiume.

Baadhi ya STI husababisha UTI kama tu, bakteria hao watasambaa kutoka ukeni hadi katika njia ya mkojo.

Mfano, vijidudu vya chlamydia husababisha STI, lakini pia vinaweza kusabisha UTI.

STI nyingi zinaenea kwa kugusana na majimaji ya sehemu za siri yenye vijidudu au kugusana ngozi kwa ngozi na ngozi ya maeneo ya viungo vya uzazi. UTI kwa kiasi kikubwa husababishwa na bakteria wanaoitwa E.Coli ambao ni bakteria rafiki wanaoishi kwenye utumbo na kwenye njia ya haja kubwa.

Vijidudu hivi kwa njia yoyote ile vikihamishwa kwenda katika maeneo mengine, husababisha maambukizi mbalimbali ikiwamo ya njia ya mkojo.

Kwa kawaida, mwili huwa na mfumo wakinga kwa ajili ya kupambambana na vimelea mbalimbali, mara tu vijidudu vinapovamia katika mrija wa mkojo, huweza kudhibitiwa haraka.

Kwa kwenda haja ndogo pekee, huweza kuwaondoa vimelea waliovamia kwenye njia ya mkojo.

Wanaume ni mara chache sana kupata UTI kwasababu wana mrija wa mkojo mrefu na huku majimaji yanayozalishwa na tezi dume huwapa mazingira magumu ya kuzaliana kwa vijidudu wanaosababisha UTI.

Lakini baadhi ya vijidudu huweza kuishinda kinga ya mwili, hivyo UTI huweza kujitokeza.

UTI huwapata zaidi wanawake, hii ni kutokana nakuwa na mrija wa mkojo mfupi na huku ukiwa jirani na njia ya haja kubwa.

Na ndio sababu wanawake hushauriwa kunawa kutoka mbele kwenda nyuma ili kupunguza hatari ya kujigusanisha na chembe chembe za kinyesi ambazo huwa na vijidudu vya E.Coli wanaosababisha UTI.

Vile vile, hutakiwa kuwa waangalifu na matumizi ya vyoo vya jumuia kwasababu kama ni vichafu, mtumiaji anaweza kupata maambukizi ya UTI.

Wanapochuchumaa ili kujisaidia baadhi ya matone hudunda sakafuni na kurudi katika njia ya mkojo yakiwa na uchafu wenye vijidudu wanaosababisha UTI.

Kwa uchache, michubuko itokanayo na kujamiana huweza kuwa mazalia ya vijidudu wanaosababisha UTI kwa wanawake na baadaye hupata nafasi ya kuvamia njia ya mkojo.

Nihitimishe kwa kusema kuwa UTI sio ugonjwa unaoenezwa kwa kujamiana kutoka mtu mmoja kwenda mwingine bali tu baadhi ya bakteria wanaosababisha STI wakivamia njia ya mkojo husababisha UTI.