Tofauti za meya, mkurugenzi zawakera madiwani Arusha

Muktasari:

Walalamikiwa kwa kushindwa kuafikiana namna ya kutatua mgogoro wa wafanyabiashara.

Arusha. Mvutano kati ya Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro (Chadema) na Mkurugenzi wa jiji, Athumani Kihamia umechukua sura mpya baada ya madiwani kuwataka viongozi hao kupatana ili kutatua kero za wananchi.

Katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika juzi, Diwani wa Kata ya Daraja Mbili, Prosper Msofe alisema madiwani wameshindwa kumaliza mgogoro wa maduka 396 katika kituo kidogo cha mabasi kutokana na viongozi hao wa jiji kutoelewana.

“Jambo la msingi ni nyie wawili mkae pamoja mje na mapendekezo yatakayomaliza mgogoro huu ambao hauna masilahi yoyote kwa wananchi wetu, bali unasababisha washindwe kufanya biashara zao kwa uhuru,”alisema Msofe.

Mgogoro huo ni kati ya wafanyabiashara waliojenga maduka hayo zaidi ya miaka 10 iliyopita na wafanyabiashara wapangaji hatua ambayo imekua ikihatarisha usalama wa mali na mapato ya halmashauri.

Pande zote mbili zimefungua kesi mahakamani wakiishtaki halmashauri ya jiji huku jitihada za kuondoa kesi hizo mahakamani zikifanyika ili kuhakikisha kunakua na maelewano na mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Kwa upande wake Meya wa Jiji, Lazaro alipendekeza iundwe kamati ya madiwani watano ili kufanya uchunguzi wa kina na kuzikutanisha pande mbili zinazopingana jambo ambalo Mkurugenzi alisema halitakua na tija kwa sababu linaweza kuleta mgongano wa kimaslahi.

Alisema amepata taarifa ya kuanzishwa kwa kamati ya maridhiano kati ya wapangaji ambao ni wafanyabiashara na waliojenga ili kumaliza tofauti zao na halmashauri itumie nafasi hiyo kuumaliza ili kutoa nafasi ya kutangazwa zabuni ya maduka hayo.

Kesi iliyofunguliwa na Dominick Mollel kwa niaba ya wenzake ilikuwa ikipinga utaratibu wa maduka hayo kupewa wafanyabiashara wengine wakati wao ni wawekezaji wajenzi walioingia mikataba na halmashauri ya jiji. pia walilalamika kutorejeshewa fedha zao za uwekezaji.

Kwa upande wake, Kihamia alisema hakuona sababu ya kuundwa kamati ya madiwani, bali ataunda timu ya wataalamu wa jiji watakazungumza na pande zote ili kuondoa kesi mahakamani na kuanza mazungumzo.

Alisema lengo la kuondoa kesi ni kupunguza migogoro kati ya jiji na wananchi pia kuhakikisha yanapatikana mapato ambayo yanatumika kutekeleza miradi ya maendeleo ndani ya jiji.