Tony Bellew kuzichapa na Oleksandr Usyk

Bondia Tony Bellew 

Muktasari:

Bondia huyo alimshinda Murat Gassiev na kutwaa taji la WBC, jambo lililoonekana kumuumiza Bellew

London, England. Bondia Tony Bellew wa Uingereza ameomba kuzichapa na Oleksandr Usyk wa Ukraine, bingwa wa Dunia uzani wa juu anayeshikilia mikanda yote inayotambuliwa na vyama vyote vinne vikubwa vya ngumi duniani, WBO, WBC, WBA na IBF.

Usyk, mwenye miaka 31, juzi Jumamosi alijiandikia rekodi ya kuwa bondia wa kwanza kushikilia kwa pamoja mataji yote manne yanayotambuliwa na WBO, WBC, WBA na IBF.

Bondia huyo alimshinda Murat Gassiev na kutwaa taji la WBC, jambo lililoonekana kumuumiza Bellew, mwenye miaka 35 ambaye aliomba apatiwe pambano ili amvue Usyk mataji hayo.

Bellew, 35, ambaye alipata kumshinda mbabe wa Dunia, David Haye mara mbili alisema licha ya umri wake kuwa mkubwa lakini anaamini atamchapa Usky na kutwaa mataji hayo.

Usyk ambaye ameshinda mapambano yake yote ya ngumi za kulipwa alisema yupo tayari kuzichapa na Bellew wakati wowote kwa kuwa yeye kazi yake ni kuzichapa na wababe.

"Nataka nicheze na Usky, nikimshinda nitaomba kuzichapa Tyson Fury na baadaye nicheze na Adonis Stevenson, ambaye alinishinda mwaka 2013, nikimshinda nitaandika historia ya kuwa bondia aliyewapiga mabondia wote aliopata kupanda naye ulingoni,” alisema.