Total kutoa mamilioni kwa vijana wenye mawazo ya biashara

Mkurugenzi wa uhusiano na sheria wa kampuni ya Total, Masha Kileo

Muktasari:

Ili kuongeza vyanzo vya mtaji, kampuni ya Total imeahidi kutoa Sh65 milioni kwa vijana watatu wenye mawazo bora ya biashara ambayo yakitekelezwa yatakuwa na mchango kwenye jamii.

Dar es Salaam. Katika kuongeza fursa za mtaji kwa wajasiriamali wadogo, kampuni ya mafuta ya Total imetangaza kutoa Sh65 milioni kwa vijana watatu wenye mawazo mazuri ya biashara.

Kiasi hicho kitatolewa kwa wabunifu hodari watakaokuwa na mawazo yanayogusa jamii kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi wa uhusiano na sheria wa kampuni hiyo, Masha Kileo amesema fedha hizo zitatolewa kwa washindi watatu wa shindano wanaloliendesha na kuwahusisha vijana wote wenye mawazo mazuri lakini wanakabiliwa na ukosefu wa mtaji kuyafanikisha.

“Mshindi kwanza atapata Sh30 milioni, wa pili Sh20 milioni na wa tatu Sh15 milioni ili kuwezesha utekelezaji wa miradi watakayoibuni hapa nchini. Washiriki watapata mafunzo maalumu juu ya uendeshaji, uangalizi na namna ya kuboresha biashara zao," amesema Kileo.

Kwa mwaka wa pili sasa, kampuni ya Total inaendesha shindano lijulinakanalo kama ‘Startupper of the year Challenge’ likiwahusisha zaidi vijana. Kwa mara ya kwanza, shindano hilo lilifanyika mwaka 2015 na Iddi Kalembo wa Mtwara akaibuka mshindi kwa mradi wake wa upigaji picha kwa simu ya mkononi hasa vijijini.

Akizungunza wakati wa uzinduzi wa shindano hilo, mkurugenzi wa fedha wa Total, Thomas Biyong amesema mbali na Tanzania, shindano hilo litafanyika katika nchi nyingine 40 barani Afrika ikiwa ni mpango wa kuinua mtaji wa wafanyabiashara wadogo.

"Miradi itapimwa kulingana na wazo la ubunifu wa asili, umuhimu kwa jaimi pamoja na uwezekano wa mradi kuwa endelevu," amesema Biyong.