Trafiki watimua mbio baada ya kushuhudia ajali ikiua ndugu

Muktasari:

  • Ajali hiyo ilitokea juzi saa 6:40 mchana wakati ndugu hao pamoja na wengine wakisafiri kwa Toyota Hiace kuelekea Shelui kumjulia hali baba yao.

Iramba. Askari wa usalama barabarani waliokuwa zamu katika kituo cha ukaguzi kilichopo Kijiji cha Kizanga wilayani hapa walitimua mbio baada ya kushuhudia ajali iliyosababisha vifo vya ndugu wawili katika ajali iliyohusisha magari matatu waliyokuwa wameyasimamisha kwa ukaguzi.

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 6:40 mchana wakati ndugu hao pamoja na wengine wakisafiri kwa Toyota Hiace kuelekea Shelui kumjulia hali baba yao.

Katika ajali hiyo, askari hao walipoteza mashine ya kutoa risiti za kielektroniki na tochi inayotumika kubaini mwendo wa magari.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema tochi ilipatikana baadaye na kwamba askari hao waliondoka eneo la tukio kwa kuhofia usalama wao. Alisema ajali hiyo ilihusisha Hiace, lori mali ya kampuni ya Mtama ya mjini Bujumbura nchini Burudi na lingine la kampuni ya Azam.

Dereva wa lori kampuni ya Mtama, Vingiyimana Victor alisema alikuwa wa kwanza kusimamishwa na askari hao na kabla hajamalizana nao, Hiace ilisimamishwa na dereva aliiegesha nyuma ya lori lake.

“Muda mfupi baadaye lilisimamishwa lori la Azam ambalo dereva wakati akifunga breki lilimshinda hivyo aliigonga Hiace iliyotupwa nje ya barabara. Baada ya hapo lori hilo liligonga kwa nyuma lori langu na kuharibika kibini,” alisema.

Mmiliki wa Toyota Hiace, Elibariki Mdede alisema walipofika eneo hilo alisimamishwa na askari hao waliomweleza kwamba alikuwa akiendesha kwa mwendokasi.

Alisema yeye pamoja na ndugu yake mmoja walishuka kwenda kuhakikisha ukweli wa taarifa hiyo eneo walipokuwa wamekaa askari na wakiwa huko, alisikia kishindo na alipogeuka aliona gari lake likiwa limegongwa kwa nyuma na lori ambalo baadaye lililigonga kwa mbele lori lingine kabla ya kupinduka kando mwa barabara.

Alisema alirudi mbio kwenye gari lake ambako alikuta ndugu yake wa kike Mwaidieli Mdede (48), akikata roho.

Alisema ndugu yake mwingine, Julius Kiula alipasuka kichwa na alifariki dunia akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Iramba iliyopo Kiomboi.