Trump atishia kufunga vyombo vya habari

Muktasari:

Rais Trump mara kwa mara amekuwa akivilenga vyombo vya habari vinavyomkosoa tangu Januari mwaka huu alipotoa hotuba yake ya kwanza kama Rais Mteule na alimlalamikia ripota wa CNN akisema anaandika habari za uongo

Washington, Marekani. Rais Donald Trump ametishia kufungia mashirika ya utangazaji kama NBC na mitandao mingine ya Marekani akidai inasambaza habari za uongo.

"Baada ya Habari za Uongo zote kutoka NBC na Mitandao yake, je ni wakati gani mwafaka kuzuia Leseni zao? Vibaya sana kwa nchi!" alihoji Trump kupitia Twitter.

Ujumbe wa Twitter wa Trump ni majibu kwa habari iliyoandikwa na NBC ikisema Trump ameamua kuongeza hazina ya silaha za nyuklia mara 10 zaidi baada ya kupata maelezo mafupi yanayoonyesha kupungua taratibu kwa hazina ya nyuklia ya Marekani tangu miaka ya 1960.

Habari hiyo iliwataja maofisa watatu waliokuwemo kwenye chumba wakati Trump akitoa kauli hiyo.

"Uongo @NBCNews imeandika habari inayosema eti mimi nataka kuongeza ‘mara 10’ hazina ya silaha za nyuklia nchini Marekani,” aliandika Trump kabla ya kutoa vitisho. “Habari ya kutunga iliyolenga kudhalilisha. NBC = CNN!"

Rais Trump mara kwa mara amekuwa akivilenga vyombo vya habari vinavyomkosoa tangu Januari mwaka huu alipotoa hotuba yake ya kwanza kama Rais Mteule na alimlalamikia ripota wa CNN akisema anaandika habari za uongo.

Fake News yaani habari za uongo ndiyo maneno anayopenda kutumia mara kwa mara tangu wakati wa uchaguzi mkuu uliomwingiza madarakani mwaka 2016 na huvilenga vyombo vyote vya habari vinavyoandika habari asizozitaka au vinapokosoa utawala wake.

Habari kuhusu shauku ya Trump kuongeza hazina ya silaha za nyuklia ilisema katika kikao hicho maofisa waliohudhuria akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson hawakuunga mkono wazo hilo na Tillerson baadaye alimwita Rais kuwa “mpuuzi.”

Tillerson alikataa wiki iliyopita kuthibitish kama alimwira rais kuwa mpuuzi na Trump amesema habari hizo ni za uongo. Katika mahojiano, Trump alisema itabidi ziangaliwe alama za IQ ya Tillerson ikiwa kweli alitoa matamshi hayo.

Hata hivyo, haijawa wazi kama Trump anaweza kufanikisha kwa urahisi kufuta leseni za utangazaji kwa mtandao wowote mkubwa eti kwa sababu tu hakubaliani na maudhui yaliyomo.