Trump, mkewe waonyesha mapenzi ya fasheni

Donald Trump na mkewe Melania wakicheza muziki katika Jengo la Makumbusho ya Taifa baada ya kuapishwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, Washington, DC juzi.   Picha na AFP

Muktasari:

  • Wimbo wao wa kwanza kwa wawili hao kucheza ulikuwa “My Way (Kivyangu)” wa mwaka 1969 uliorekodiwa na gwiji wa muziki, Frank Sinatra. Lakini katika sherehe ya juzi, kibao hicho kiliimbwa na nyota wa muziki wa jazz, Erin Boheme.

Washington. Donald Trump na mkewe, Melania juzi walilionyesha jiji la Washington mvuto wa familia yao  wakati walipopanda kudansi kwenye jukwaa lililopambwa kwa taa za rangi nyekundu, nyeupe na bluu ambazo ni za bendera ya Marekani.

Wimbo wao wa kwanza kwa wawili hao kucheza ulikuwa “My Way (Kivyangu)” wa mwaka 1969 uliorekodiwa na gwiji wa muziki, Frank Sinatra. Lakini katika sherehe ya juzi, kibao hicho kiliimbwa na nyota wa muziki wa jazz, Erin Boheme.

Melania Trump alivutia waalikwa kwenye sherehe hiyo alipoibuka na gauni lake jeupe la kung’aa, lililoacha mabega wazi, lakini lenye mikono ya mchinjo, na refu hadi kufikia kifundo cha mguu, lakini likiwa na mpasuo unaofikia juu kidogo ya goti.

Hafla hiyo ilikuwa ya kusherehekea kukabidhiana madaraka kwa amani baada ya rais aliyemaliza muda wake, Barack Obama kumpisha Trump. Hafla hiyo ya burudani hufanyika kuzindua kipindi cha rais mpya ambaye huitumia kuonyesha mapenzi yake katika mavazi, muziki na dansi.