Masenta waondoa mkwamo wa matumizi ya serikali

Muktasari:

Wabunge 33 wa Democrat waliungana na wenzao 48 wa Republican kuridhia kuongeza muda wa muswaada wa matumizi ya serikali kuu hadi Februari 8.

Washington, Marekani. Rais Donald Trump alitia saini Jumatatu muswada kuidhinisha matumizi ya serikali ya shirikisho hivyo kuhitimisha mkwamo wa saa 69 baada ya maseneta wa chama cha Democratic kupiga kura kuridhia kwa muda shughuli za serikali ziendelee.

Makubaliano ya kupitisha mpango wa matumizi ya serikali uliridhiwa na wabunge wa vyama vyote baada ya kufungwa kwa baadhi ya shughuli Ijumaa usiku.

Wabunge 33 wa Democrat waliungana na wenzao 48 wa Republican kuridhia kuongeza muda wa muswaada wa matumizi ya serikali kuu hadi Februari 8.

“Leo ni siku ya kushereheka,” alisema Seneta Susan Collins wa Maine wa Republican. “Serikali inapofungwa, inabainisha kushindwa kutawala.” Baadaye Trump alitia saini akiwa ofisini kwake.

Kura ya kuongeza muda ilifungua ukurasa muhimu kwa mamia na maelfu ya wafanyakazi kurejea kazini Jumanne na hivyo kuiokoa serikali katika aibu.

Kiongozi wa walio wengi bungeni, Mitch McConnell wa Kentucky aliwahakikishi wabunge wa Democratic kuwa watazungumzia masuala mbali ya uhamiaji, ikiwemo maelfu ya wahamiaji ambao hawana vibali, ambao waliingizwa Marekani kama watoto ambao hali yao ya baadaye ndiyo suala kuu linalojadiliwa baada ya Trump kuamua kufuta programu ambayo inawaruhusu kusoma na kufanya kazi Marekani.