Trump atolewa mbio kuepuka kupigwa risasi

Muktasari:

Maofisa usalama walilazimika kumtoa Trump jukwaani juzi kwa kukimbia naye, huku wakiwa wamemzingira hadi nje ya ukumbi wa mikutano alikokuwa akifanya kampeni.

Nevada. Mgombea urais wa Marekani kupitia Chama cha Republican, Donald Trump ametolewa jukwaani wakati wa mkutano mjini Reno, Nevada, kufuatia kitisho cha usalama wakati akiwa kwenye kampeni za kuelekea Ikulu ya White House.

Maofisa usalama walilazimika kumtoa Trump jukwaani juzi kwa kukimbia naye, huku wakiwa wamemzingira hadi nje ya ukumbi wa mikutano alikokuwa akifanya kampeni.

Tukio hilo lilitokana na tishio la mmoja wa watu waliokuwa kwenye mkutano huo kwamba angemshambulia Trump kwa risasi.

Maofisa usalama hao walifanikiwa kumkamata mtu huyo ambaye alikuwa kwenye umati baada ya kumtilia shaka na kuanza kumkagua hali ambayo ilizua tafarani.

Hata hivyo, kabla ya kumkamata mtuhumiwa, wafuasi wa Trump waliokuwa wakimsikiliza walianza kumnyoshea vidole kijana huyo wakidai anataka kumdhuru kwa risasi mgombea huyo.

Baadhi ya mtuhumiwa kukamatwa na hali kutulia, Trump huku akionekana mtulivu alirejea jukwaani na kuendelea na kampeni.

Mjini Philadelphia, mwanamuziki wa miondoko ya pop, Kate Perry alitumbuiza katika mkutano wa kampeni wa Hillary Clinton wa Democtaric, akiwa na nyota wengine wanaoungana na mgombea huyo kwa lengo kupata kura kutoka kwa vijana. “Wakati watoto wako na wajukuu zako watakapokuuliza ulifanya nini mwaka 2016 wakati kila kitu kilikuwa hatarini, nataka uwe na uwezo wa kusema kuwa ulipiga kura kwa ajili ya Marekani iliyo bora na imara zaidi,” alisema Clinton.

 

Clinton afanya kampeni kwenye mvua

Muda mfupi kabla Clinton hajapanda jukwaani mjini Pembroke Pines, jimboni Florida, mvua ilinyesha. Watu waliendelea kumsubiri mgombea huyo, huku wakitoa miavuli na wengine kujifunika mifuko ya plastiki inayotumika kukusanya taka.

“Nimevutiwa kuwa hapa na kundi hili maridhawa, ije mvua au jua mko tayari,” alisema Clinton. Lakini alifupisha hotuba yake baada ya kulowa na mvua akisema: “Sidhani kama nahitaji kuwaambia mambo yote mabaya kuhusu Trump.”

Uchunguzi wa maoni unaonyesha Clinton bado ana nafasi katika majimbo yanayoweza kuwa muhimu kuamua matokeo ya uchaguzi huo utakaofanyika baadaye mwezi huu.

Matokeo ya uchunguzi wa maoni ulioendeshwa na mashirika ya McClatchy na Marist yaliotolewa wiki iliyopita (Jumamosi) yalionyesha Clinton akiongoza kwa pengo la asilimia moja ikilinganishwa na asilimia sita Septemba.

Uchunguzi wa Reuters na Ipsos siku hiyo hiyo ulionyesha Clinton akiwa mbele kwa tofauti ya asilimia nne kitaifa ikilinganishwa na asilimia tano aliyokuwa nayo Ijumaa iliyopita.

Uchaguzi wa mapema ulianza Septemba na kampuni ya Catalist, inakadiria kuwa zaidi ya kura milioni 30 zimepigwa katika majimbo 38. Kuna takriban watu milioni 225.8 wenye vigezo vya kupiga kura nchini humo Novemba 8, mwaka huu.

Jumamosi iliyopita ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya upigaji kura wa mapema katika kaunti nyingi za Florida.

Katika maktaba ya JFK mjini Hialeah, Florida, watu walipanga foleni nje kwa ajili ya uchaguzi wa mapema. Eneo la karibu na hapo wafuasi wa wagombea wote walikuwa wakipeperusha vibao na kuimba nyimbo, wakiwataka madereva waliokuwa wakipita kupiga honi. “Tunahitaji mtu aingie na kusafisha nyumba,” alisema raia wa Marekani mwenye asili ya Cuba, Ariel Martinez mwenye umri wa miaka 42 na mfuasi wa Trump.