Tucta: Tuko tayari kuhamia Dodoma

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya

Muktasari:

Mgaya alitoa kauli hiyo jana muda mfupi baada ya kufungua mkutano wa Tano wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) ambao unaendelea mjini hapa.

Dodoma. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya amesema wako tayari kuelekea Dodoma.

Mgaya alitoa kauli hiyo jana muda mfupi baada ya kufungua mkutano wa Tano wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) ambao unaendelea mjini hapa.

Alisema mpango wa Serikali kuhamia Dodoma ulianza siku nyingi tangu enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza, hivyo akawabeza wanaosema Serikali imekurupuka.

“Hakuna kukurupuka hapa jamani, tangu awamu ya kwanza mpaka leo inakuwaje ni kukurupuka kama si kwamba tumechelewa?” alihoji Mgaya.

Alisema Tucta ina majengo mjini Dodoma na hivyo mahali pa kufikia wanapo, kinachosubiriwa sasa ni Serikali kuhamia, nao wafuate.