Tucta waipongeza Serikali kulipa madeni

Muktasari:

Hivi karibuni Tucta iliipelekea Serikali mapendekezo 11 yanayotakiwa kufanyiwa kazi kuboresha mazingira ya wafanyakazi nchini ikiwamo malipo ya malimbikizo ya madai.

 Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limeipongeza Serikali kwa uamuzi wa kulipa malimbikizo ya madai ya watumishi wa umma wakiwamo walimu kwa kuwa itawaongezea ari ya kufanya kazi.

Hivi karibuni Tucta iliipelekea Serikali mapendekezo 11 yanayotakiwa kufanyiwa kazi kuboresha mazingira ya wafanyakazi nchini ikiwamo malipo ya malimbikizo ya madai.

Juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema malimbikizo ya madai ya watumishi wa umma 27,389 yenye thamani ya Sh43.39 bilioni yatalipwa pamoja na mshahara wa Februari, 2018 kwa mkupuo.

Malipo hayo yatajumuisha madai ya watumishi ya zaidi ya miaka 10 iliyopita huku majina ya watakaolipwa ilielezwa yangeanza kutangazwa jana kwenye vyombo vya habari.

Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahaya Msigwa alisema hatua hiyo itamaliza kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi na kuongeza ari ya kazi.

Alisema madai hayo ilikuwa moja ya kero zilizokuwa zinalikabili kundi hilo kwa muda mrefu bila kupata ufumbuzi.

“Wafanyakazi wakiwamo walimu walikuwa na madai ya muda mrefu sana na pengine walishakata tamaa, hatua hii ya kuwalipa ni nzuri na tuipongeze Serikali, tunasubiri mwisho wa mwezi kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hii,” alisema Dk Msigwa.

Alifafanua kuwa elimu ni kati ya sekta nyeti ambazo madai yake kwa namna fulani yalikuwa yanaweza kuchangia kushuka kwa kiwango cha elimu kutokana na kukosa imani na morali ya kufanya kazi kutokana na malimbikizo ya madeni yao.

Dk Msigwa alisema kiuhalisia ufaulu kwa shule binafsi unachangiwa na namna wanavyowajali walimu wao.

“Unajua kinachosababisha ufaulu mkubwa wa wanafunzi katika shule binafsi ni motisha kwa walimu kwa hiyo kuwalipa madai yao itasaidia kuinua elimu,” alisema.

Dk Msigwa alisema kwamba wafanyakazi wanapokosa matumaini ya malipo yao wanapunguza morali ya kazi na kwa kundi la walimu, matokeo yake huja kuonekana baadaye.

“Morali ya walimu ikishuka inaathiri ufundishaji na mwisho wa yote huwa kuna ufaulu mdogo wa mitihani ya kitaifa,” alisema.