UCHAGUZI KENYA: Waziri awahakikishia usalama wageni

Kaimu Waziri wa Usalama, Dk Fred Matiang’i

Muktasari:

Akizungumza baada ya kukutana na mabalozi wa mataifa ya kigeni nchini humo walioongozwa na Balozi wa Zimbabwe, Kelebert Nkomani, kaimu Waziri wa Usalama, Dk Fred Matiang’i alisema idara ya usalama imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba amani inadumishwa kabla na baada ya uchaguzi.

Nairobi. Wakati nchi za Marekani na Uingereza zimewatahadharisha raia wake, Serikali ya Kenya imeyahakikishia mataifa ya kigeni kuwa uchaguzi ujao utakuwa wa amani na utulivu.

Akizungumza baada ya kukutana na mabalozi wa mataifa ya kigeni nchini humo walioongozwa na Balozi wa Zimbabwe, Kelebert Nkomani, kaimu Waziri wa Usalama, Dk Fred Matiang’i alisema idara ya usalama imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba amani inadumishwa kabla na baada ya uchaguzi.

“Tumewaonyesha mipango yetu ya usalama na tumejibu maswali waliyokuwa nayo kuhusiana na maandalizi ya usalama wakati huu wa uchaguzi,” alisema Dk Matiang’i.

Alisema maofisa wa usalama wako tayari kuwezesha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuandaa uchaguzi huru na wa haki kwa kuhakikisha kuwa Wakenya wanapiga kura kwa amani.

Waziri Matiang’i alitoa hakikisho hilo siku mbili baada ya mataifa ya Uingereza na Marekani kuelezea uwezekano wa kutokea kwa vurugu kabla na baada ya uchaguzi.

Mataifa hayo mawili pia yalionya raia wake kujiepusha na mikutano ya kisiasa ikiwamo kutosafiri katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

“Uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani utafanyika Agosti 8. Kuna uwezekano wa kutokea kwa machafuko kabla na baada ya uchaguzi. Kuweni makini kwa kufuatilia vyombo vya habari vya Kenya na kimataifa. Mnapoona dalili za vurugu ondokeni mara moja,” ilitahadharisha taarifa iliyotolewa na Uingereza kwa raia wake.

Uingereza pia ilionya raia wake kutotembelea maeneo yaliyoko kilomita 60 kutoka mpaka wa Kenya na Somalia, baadhi ya maeneo katika Kaunti ya Lamu, Tana River na Garissa kutokana na hofu ya uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi.

Pia, Marekani iliwataka raia wake kujiepusha na makundi ya watu au waandamanaji.

“Kenya imekuwa ikishuhudia vurugu za kabla ya uchaguzi tangu 1992 na baada ya uchaguzi wa 2007. Kuna uwezekano wa kuzuka kwa vurugu kabla au baada ya uchaguzi ujao.

Hivyo tunawashauri raia wa Marekani kujiepusha na makundi ya watu kwani yanaweza kuwa na magaidi,” ilisema taarifa ya Marekani.

Dk Matiang’i, hata hivyo, alisema kuwa serikali itatuma maofisa wa kutosha wa usalama katika maeneo ambayo huenda yakakumbwa na vurugu za baada ya uchaguzi.