UDSM kufanya utafiti nyayo za binadamu wa kale

Muktasari:

Makumbusho ya Olduvai Gorge yaliyopo katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha baadhi ya vilivyomo ndani yake ni nyayo za binadamu wa kwanza na fuvu la binadamu wa kale.

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitivo cha ikolojia kinafanya utafiti katika Bonde la Oldupai Gorge, kuangalia maisha halisi ya binadamu wa kale.

Makumbusho ya Olduvai Gorge yaliyopo katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha baadhi ya vilivyomo ndani yake ni nyayo za binadamu wa kwanza na fuvu la binadamu wa kale.

Utafiti huo unaelezwa kuwa utaleta matokeo chanya nchini Tanzania na utagusia zaidi mabadiliko ya binadamu vizazi na vizazi ukilenga zaidi binadamu alipoanzia, tabia zake katika tamaduni za kale, alichokula, mpangilio wake wa mlo na namna ya utafutaji wake wa chakula.

Hayo yamesemwa leo Julai 12 na Rasi wa Ndaki ya Insia, Dk Rose Upor wakati akizindua warsha iliyowahusisha wadau mbalimbali kutoka idara ya akiolojia, wadau kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Chuo Kikuu cha Calgary.

“Zaidi ni mageuzi ya binadamu tulipoanzia na tabia zetu katika tamaduni zetu za zamani za kale, kutafiti walikula nini, walilima nini kipindi kile na jinsi ambavyo wameweza kubadilika kadri miaka ilivyokuwa inazidi kwenda kwa kuangalia mabadiliko ya hali ya hewa kulingana na maeneo yale,” amesema Dk Upor.

 Amesema utafiti huo utasaidia katika kujifunza kwa ajili ya kujiandaa kwa maisha ya baadaye na kuelewa mwelekeo wa binadamu wa sasa na kwamba, tayari kwa sasa utafiti umeanzia Oldupai George na wataendelea katika maeneo mengine.

 Dk Upor amesema utafiti huo unafanywa na wafanyakazi kutoka idara ya Ndaki ya Insia wawili ambao kwa sasa wanasomea shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Calgary.

Katika warsha hiyo, wakufunzi kutoka UDOM na Chuo Kikuu cha Calgary wametoa mafunzo ya namna ya uandishi wa maombi mbalimbali katika kutafuta fedha za kufanyia tafiti.

Baada ya warsha hiyo, wadau walioshiriki watasafri pamoja kuelekea Makumbusho ya Oldupai Gorge kwa ajili ya kuendelea na utafiti.