UDSM yawatadharisha wanafunzi na matapeli

Mkurugenzi wa Shahada za awali wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Allen Mushi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu matapeli wanaowaibia wanafunzi fedha kwa madai ya kuwa wakiwalipa kwa miamala ya simu watapatia fumo za udahili za chuo hicho. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kompyuta Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Elliamini Minja. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Uongozi wa UDSM katika siku za karibuni umekuwa ukipokea malalamiko ya baadhi ya wanafunzi wanaodaiwa kutapeliwa katika udahili 

Dar es Salaam.  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetoa tahadhari kwa wanafunzi wanaoomba kudahiliwa na chuo hicho kuwa makini baada ya kuibuka wimbi la matapeli. 

Tangu shughuli ya udahili ianze Julai 24, mwaka huu, chuo hicho kimekuwa kikipokea wanafunzi wengi waliotapeliwa. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Julai 28,  Mkurugenzi wa Shahada za Awali, Profesa Allen Mushi amesema wanafunzi hao wanatapeliwa kwa kutuma fedha za udahili baada ya kupata ujumbe wa meseji kwenye simu zao za mkononi na kuambiwa fomu za kujiunga zinapatikana chuoni jambo ambalo si sahihi. 

Profesa Mushi alisema kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), maombi yote yanafanyika kwa njia ya mtandao.