UHANDISI JENI: TEKNOLOJIA MPYA KWA KILIMO CHA KISASA

Muktasari:

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kusambaa kwa kasi kwa magonjwa, milipuko ya magonjwa mapya na wadudu waharibifu wa mazao.

Dar es Salaam. Mabadiliko ya tabianchi yameibua changamoto mpya katika sekta ya kilimo.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kusambaa kwa kasi kwa magonjwa, milipuko ya magonjwa mapya na wadudu waharibifu wa mazao.

Mabadiliko ya tabianchi yamehusishwa pia na usugu wa wadudu na kubadilika kwa misimu ya mwaka. Wataalamu wa hali ya hewa, sawa na ilivyo kwa wakulima wamekuwa wakishindwa kuitabiri kwa uhakika.

Yubo Mbwambo ni mkulima wa mahindi katika Kata ya Nyehunge katia Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza, anasema mahindi ndilo lililokuwa zao tegemeo ambalo liliwapatia chakula baada ya muhogo ambao ulikuwa zao lao kuu kushambuliwa zaidia na magonjwa, lakini sasa kwenye shamba lake la mahindi la eka moja hana uhakika wa kupata hata magunia matano kutokana na wadudua aina ya bungua kushambulia shamba zima

Matatizo ya magonjwa hayaishii kwa wakulima wa mazao ya chakula pekee, bali yanaathiri yale ya biashara kama pamba na hivyo kuwakosesha tija wakulima na kujikuta wakipata hasara kila mwaka.

Mfano mzuri ni kwa Maguha Mayala ambaye ni mkulima wa pamba katika Kijiji cha Kikumbi, Kata ya Lugunga wilayani Mbogwe mkoani Geita anayelalamika kuwa dawa za pamba kwa sasa haziui wadudu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Anasema analazimika kupuliza dawa mara saba hadi 10 mpaka kuvuna na hupata kilo 600 kwa eka moja kitu ambacho ni hasara kubwa kwake.

Mtafiti aliyebobea kwenye tafiti ya bioteknolojia nchini, Dk Emaroid Mneney anasema usugu wa wadudu dhidi ya viuatilifu vingi kwa sasa ni mkubwa na ongezeko la magonjwa ya mimea huchangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko hayo.

‘Uhandisi jeni ni teknolojia inayotumia michakato ya kibaolojia kuzalisha mbegu za mazao au mimea, kunaweza kuwapo na sifa ya kukinzana na magonjwa, kustahimili ukame na kupambana na wadudu waharibifu wa mazao. Teknolojia ya uhandisi jeni inapunguza matumizi ya dawa za kemikali na pia huongeza tija katika kilimo,” anasema Dk Mneney.

“Kiumbe kinachoimarishwa kwa njia ya uhandisi jeni hutambulika zaidi kama GMO, kifupi cha maneno ya Kiingereza cha Genetically Modified Organism”.

Nafasi ya Uhandisi Jeni kwa Mkulima

Kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni watafiti wanaweza kuzalisha mbegu za zao lolote ambalo litakuwa na uwezo wa kutoa mazao kwa wingi kuliko kawaida na hivyo kumwezesha mkulima kupata mavuno mengi shambani.

Pia, teknolojia ya uhandisi jeni inaweza kutumika kuzalisha mimea yenye uwezo wa kujikinga yenyewe dhidi ya magonjwa na wadudu, hivyo kumfanya mkulima kutotumia viuatilifu.

Hivi sasa watafiti wa kilimo nchini wanatafiti uzalishaji wa muhogo utakaokuwa na uwezo wa kujikinga dhidi ya magonjwa ya batobato na michirizi kahawia.

Utafiti mwingine nchini ni ule wa kuzalisha mahindi yanayostahimili ukame, mvua ya muda mfupi na mkulima bado anaweza kuvuna mavuno mengi.

Mradi huo pia unatafiti aina ya mahindi yatakayokuwa na uwezo wa kujikinga wenyewe dhidi ya bungua na michirizi ya mahindi wakati huohuo yakistahimili hali ya ukame.

Serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba ilielekeza watafiti kuangalia uwezekano wa kuzalisha mbegu za pamba zitakazoweza kupambana na wadudu wanaoshambulia zao hilo.

“Pamba ya Bt imefanya vizuri huko kwingine, watafiti wetu wafanye jitihada za haraka ili wakulima wa Tanzania nao wafaidi,” alisema Dk Tizeba.

Lishe na changamoto zake

Tatizo la lishe duni na upatikanaji wa lishe ni changamoto kubwa kwa Taifa. Mchango wa uhandisi jeni unahitajika ili kuzalisha mazao ambayo yameongezewa virutubisho vinavyohitajika mwilini, hasa kwa chakula cha Mtanzania wa kawaida mfano mchele, muhogo, ndizi na mtama.

Kufuatia hali ya mvua kutokuwa ya uhakika na unapatikana kwa vipindi vifupi, watafiti wanaweza kutumia teknolojia ya uhandisi jeni kuzalisha mbegu za mazao ambayo yatastahimili ukame na hivyo kulikinga Taifa na janga la njaa, hasa nyakati za mabadiliko ya tabia nchi.

Pia, teknolojia ya uhandisi jeni inawezesha kuzalisha mifugo yenye kustahimili magonjwa na kutoa mazao bora.

Wakulima wanaofaidi teknolojia

Wakulima zaidi ya milioni 16.7 kutoka mataifa mbalimbali wanaomiliki zaidi ya eka 452 milioni za mazao ya kilimo kilichewezeshwa na teknolojia ya uhandisi jeni wanafaidi teknolojia ya uhandisi jeni.

Nchi 10 bora ambazo wakulima wake wanatumia teknolojia hii ni Marekani eka 172.5 milioni, Brazil eka 75 milioni, Argentina eka 59 milioni, India eka 6.5 milioni, Canada eka 26 milioni, China eka 10 milioni, Paraguay eka 7 milioni, Pakistan eka 6.5 milioni, Afrika Kusini eka 6 milioni na Uruguay eka 3 milioni.

Mazao makuu yanayolimwa kwenye nchi hizo ambayo yameshafanyiwa uhandisi jeni ni soya, mahindi, pamba, biringanya, mapapai, zao la mafuta ya kula la kanola, viungo pamoja na nyanya.Kwa upande wa Afrika, nchi ya Afrika Kusini inalima mahindi na pamba huku Burkina faso na Sudani zikilima pamba.

Nchi zingine za Afrika zilizofikia hatua za mwisho na zitaanza kuzalisha mazao yaliyoimarishwa kwa teknolojia ya uhandisi jeni ni Camerou (pamba); Ghana (pamba, mpunga na kunde), Kenya (muhogo, pamba na mahindi), Uganda (ndizi, pamba, mpunga na muhogo), Nigeria (kunde, pamba na muhogo), Malawi (pamba) na Afrika Kusini inatarajia kuongeza mazao ya viazi mviringo na miwa.

Tanzania kwa sasa ni mtumiaji wa bidhaa zitokanazo na bidhaa za GMO hasa nguo tunazoingiza nchini kutoka China, India, Pakistan, Marekani, Afrika Kusini na nchi nyingine zinazopata malighafi ya pamba kutoka kwenye mataifa yanayozalisha pamba kwa teknolojia ya kisasa.

Watafiti wanasema ili mkulima wa Tanzania wa mahindi kama Mbwambo wa Buchosa apate mahindi ya kutosha na kupambana na mdudu hatari wa bungua wa mahindi anahitaji kupata mbegu za kisasa zilizoboreshwa kwa kutumia teknolojia hiyo ambazo zinakinga zenyewe dhidi wa mdudu, lakini pia vivyo hivyo kwa mkulima wa pamba kama Mayala wa wilayani Mbogwe kupata pamba ya Bt ambayo anaweza kuipulizia dawa mara moja au mbili hadi kuvuna na kumpatia tija.

Mafanikio makubwa kwa wakulima na nchi katika uzalishaji yatafikiwa endapo Serikali itatumia ufunguo wake wa kuweka mazingira mazuri na wezeshi kisera pamoja na kimfumo.

Na endapo hili litafanyika, basi wakulima wa pamba na mahindi kufikia mwaka 2020 watakuwa wamefaidi wakati wale wa muhogo watasubiri hadi mwaka 2021.