Monday, December 18, 2017

Agizo la Magufuli lafanyiwa kazi

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Jumuiya ya Vijana CCM (UVCCM) imetekeleza agizo la Rais John Magufuli kwa kuhakiki  kura zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa jumuiya hiyo wiki iliyopita na kujiridhisha na washindi waliotangazwa.

Uchaguzi huo uliofanyika ulimchagua Kheri James kuwa mwenyekiti mpya wa umoja huo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 18  katika ukumbi wa Kikwete , Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamid Shaka amesema uhakiki huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli lililotaka kujiridhisha kama wametenda haki kwa kufanya uhakiki wa kuhesabu upya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo.

“Naomba kuwajulisha leo   tumekamilisha zoezi la uhakiki wa kura ambazo zilipigwa tarehe 10 (Desemba 10). Tumekuwa na wenzetu wa vyombo, tumehakiki zoezi limekwenda vizuri,”amesema.

Amesema  baada ya hakiki huo wamejiridhisha kuwa matokeo ya wagombea waliowania nafasi mbalimbali ni halali na kwamba waliochaguliwa wamechaguliwa kihalali.

“Umoja wa vijana umesimamia uchaguzi kwa haki na tuna nia ya dhati ya kumuunga mkono Rais Magufuli na hakuna sehemu tulifanya ubabaishaji wala hakuna sehemu moja ama kwa namna moja ama nyingine tumemdanganya Rais,”amesema.

Amesema wamekamilisha tathimini hiyo na kuwasilisha katika mamlaka husika chama hicho . Shaka aliyekuwa ameongozana na watendaji wake, amesema kila jambo linalohusu uchaguzi huo walijiandaa vizuri kwa kuzingatia maslahi ya jumuiya hiyo na Taifa.

Amewataka wanachama wa jumuiya hiyo kuungana kwenye kujenga umoja, mshikamano katika kufanya mageuzi ambayo yatalenga kwenye utawala, mfumo, utendaji na siasa.