UVCCM yaanzisha vita wasiotekeleza ahadi
Muktasari:
Mwakifuna alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao na Mwenyekiti wa UVCCM wa mikoa ya Songwe na Mbeya, Aman Kajuna aliyetembelea wilayani hapa kukagua miradi ya vijana.
Ileje. Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani hapa, John Mwakifuna amesema chama hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na baadhi ya viongozi wake kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi.
Mwakifuna alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao na Mwenyekiti wa UVCCM wa mikoa ya Songwe na Mbeya, Aman Kajuna aliyetembelea wilayani hapa kukagua miradi ya vijana.
“Tunapata wakati mgumu kwa wapiga kura na kuhojiwa maswali magumu kutokana na wagombea waliopita katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutotekeleza ahadi na hasa zinazohusu kuboresha miundombinu ya barabara, zahanati kila kijiji na pembejeo za kilimo kutofika kwa wakati,” alisema.
Alisema baadhi ya wenyeviti wa vijiji, madiwani na wabunge hawawatembelei wananchi kujua kero zao na kuzitafutia majawabu.