UVCCM yamwagia sifa Rais Magufuli, yamtwisha zigo lingine -VIDEO

UVCCM wampongeza Magufuli

Muktasari:

  • Ripoti ya uchunguzi wa mchanga ilitolewa jana Ikulu.

Dar es Saalam. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umeitaka serikali kupitia upya mikataba yote ya madini ili kubaini kama ina manufaa na maslahi kwa umma.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka ameyasema  hayo wakati sherehe za kumpongeza Rais John Magufuli kwa kubaini madudu kupitia kamati aliyoiunda kuchunguza mchanga wa madini.

Shaka amesema UVCCM inaunga mkono jitihada hizo kwa sababu ndivyo inavyoelekezwa kwenye ilani ya CCM ambayo anaisimamia.

Mbali na  pongezi hizo Shaka amesema  ipo haja kwa Rais Magufuli kuwaweka pembeni wasaidizi wake ambao bado wanaonekana kuwa na kigugumizi katika kuwatumikia wananchi.

"Hatuko tayari na hatutakubali kushuhudia tena Tanzania ikirejea katika zama za kiza kinene cha ukwapuaji mali, ulaji na wizi wa mali za umma."

"Tunaishauri Serikali iendelee na mikakati yake ya kuhakikisha, ukwapuaji,ubabaishaji, wizi na ufisadi wa mali za serikali vinakomeshwa mara moja,"amesema Shaka.