UWT Ubungo watembelea Hospitali ya Kimara

Katibu wa UWT Amina Makilagi akimkabidhi mganga mfawidhi wa hospital ya kimara Alfonsina Mbinda vifaa vya tiba ikiwa ni maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.

Muktasari:

  • Wameamua kutembelea hospitali hiyo kwa kuwa iko wilaya mpya na inahudumia idadi kubwa ya wakazi wa Kimara.

Dar es salaam. Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Ubungo wameadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kutembelea Hospitali ya Kimara na kutoa msaada wa vitu mbalimbali.

Katika maadhimisho hayo ambayo hufanyika Machi 8 kila  wanawake hao waliadhimisha kwa kufanya usafi na kugawa vifaatiba.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo leo Machi 8, katibu wa UWT Taifa, Amina Makilagi amesema kwa kuwa yeye ni mbunge atahakikisha kwenye bunge lijalo anawakilisha maombi kwa waziri husika ili hospitali hiyo ipanuliwe.

“Nashukuru kutembelea hii hospitali nakujionea changamoto mbalimbali ikiwamo kutokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa  na kuhudumia idadi kubwa, niwahakikishie nitamfikishia kero hii waziri husika wakati wa kikao cha bunge lijalo,” amesema.

Makilagi ambaye ni mbunge wa viti maalumu, amesema wameamua kutembelea hospitali hiyo kwa kuwa iko wilaya mpya na inahudumia idadi kubwa ya wakazi wa Kimara.

Naye mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Alfonsina Mbinda amesema changamoto kubwa za hospitali hiyo ni upungufu wa watumishi na uhaba wa vyumba vya wagonjwa.