UWT yawakomalia waliokopa Benki ya Wanawake

Muktasari:

  • Mikopo ambayo benki hiyo inawadai wateja wake ni Sh6.79 bilioni

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM, Gaudentia Kabaka amewapa siku sita wadaiwa sugu wapatao 7,065 wa Benki ya Wanawake (TWB) kulipa madeni yao.

Kabaka amechukua hatua hiyo kufuatia agizo la Rais John  Magufuli alilolitoa Desemba 8, 2018 alipokuwa akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa tisa umoja huo mjini Dodoma kuutaka uongozi mpya wa UWT kukutana na uongozi  benki hiyo kuangalia inaweza vipi kusaidia iwafikie wanawake wengi na kupata mikopo kwa riba nafuu.

Akizungumza leo Machi 7, 2018 amesema baada ya agizo hilo la rais, alikutana na uongozi wa benki hiyo pamoja na bodi yake na miongoni mwa mambo waliyojadili ni pamoja na kuifuta mikopo chechefu inayoikabili benki hiyo.

Amesema iwapo wadaiwa hao sugu hawatalipa katika siku hizo sita (kuanzia leo) mali zao walizoweka dhamana zitapigwa mnada.

Ametaja mikopo ambayo benki hiyo inawadai wateja wake kuwa ni Sh6.79 bilioni.

Amesema wadaiwa hao ni wengi mno, hivyo wanahatarisha uhai wa benki hiyo.

"Sisi umoja wa wanawake na wanawake wote nchini hatukubali na hatuko tayari kabisa kuona watu wachache wakiwamo wanawake wenzetu kuitumia benki hii kwa kujinufaisha wao binafsi," amesema Kabaka.

Amebainisha kuwa wanapenda kuona mikopo hiyo inarudishwa kwa wakati ili wengine waendelee kukopa bila matatizo.

Hata hivyo, Kabaka amebainisha kuwa hadi kufikia Desemba 31, 2017 jumla ya wajasiriamali 8,123 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya Sh11.87 bilioni, kati yao wanawake ni 6,286 (sawa na asilimia 77).