Uagizaji wa dawa nje wagharimu Sh224 bil

Muktasari:

  •  Serikali yatoa mwongozo mpya wa dawa

Serikali imesema kila mwaka inapoteza mapato ya dola 100 milioni (Sh224 bilioni)kwa kuagiza dawa nje ya nchi.

Pia, imesema uagizaji wa dawa hizo nje ya nchi unatokana na kukosekana kwa viwanda vya kuzalisha dawa na vifaavita nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa toleo la tano la mwongozo wa matibabu nchini na orodha ya taifa ya dawa muhimu jana, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali itaboresha upatikanaji wa dawa kwa kuimarisha sekta ya viwanda.

Ummy alisema kuboreshwa kwa sekta hiyo kutapunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza dawa kutoka nje, badala yake kujikita katika kuimarisha uzalishaji wa dawa kwenye viwanda vya ndani.

Mwongozo mpya

Akizungumzia mwongozo huo, Ummy alisema umezingatia mabadiliko ya kitabibu na kwamba toleo hilo la tano litaimarisha huduma ngazi za zahanati na vituo vya afya.

Alizitaja baadhi ya dawa hizo kuwa ni zinazotibu magonjwa ya kisukari, Ukimwi, kifua kikuu, malaria na magonjwa mengineyo.

Ummy alisema katika kudhibiti kuenea kwa usugu wa vimelea vya magonjwa ya kuambukiza, mwongozo umefuata maelekezo yaliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambayo dawa aina ya antibiotiki zitatakiwa kutumika kwa umakini mkubwa. “Katika mwongozo huu wa dawa za antibiotiki zimegawanywa makundi matatu ya access, watch na reserve, antibiotiki za kundi la kwanza zimeainishwa kutumika katika ngazi zote za kutolea huduma nchini,” alisema Ummy.

Alisema kundi la pili hazitaruhusiwa kutumika ngazi za zahanati na vituo vya afya, bali hospitali za halmashauri.

“Dawa za antibiotiki kundi la tatu zitaruhusiwa kutumika hospitali za rufaa za kanda, hospitali ya taifa na hospitali maalumu, hivyo nasisitiza tuzingatie mgawanyo huu tunaponunua au kuagiza dawa kutoka Bohari ya Dawa (MSD),” alisema Ummy.

Naye mganga mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi alisema mwongozo huo utatoa orodha ya dawa ambazo zitakuwa zikitumika nchini. “Katika uandaaji wa mwongozo huu na orodha hii ya dawa tumejitahidi kuwashirikisha wadau kadri ambavyo imewezekana, mwanzoni kulikuwa na wataalamu wa magonjwa mbalimbali ambao wao ndiyo walikuwa wakiainisha namna ya kutibu magonjwa haya na dawa ambazo zilitakiwa zitumike, lakini kwa sasa kumekuwa na mabadiliko kadhaa,” alisema.

Mwakilishi wa mradi wa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Uswisi, Fiona Chilunda alisema kuwapo mwongozo ni jambo moja na kutumika ni jambo jingine.

“Nitoe rai kwa wadau wote uwe mhudumu wa afya au mtumia dawa, ni muhimu kuzingatia matumizi ya dawa yaliyo sahihi, tuache kutumia dawa kiholela,” alisema.