Uamuzi Chadema waibua mjadala

Muktasari:

  • Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitaja sababu tatu za kutoshiriki chaguzi hizo ikiwamo ya kutoandikishwa kwa wapigakura wapya tangu 2015, hujuma, kutumika kwa nguvu ya vyombo vya dola na kutishwa kwa wapigakura.

Dar es Salaam. Uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kutoendelea kushiriki chaguzi ndogo zote zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi sasa, umeungwa mkono na viongozi wa vyama vitatu vya upinzani huku baadhi ya wasomi wakishauri kisisusie.

Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitaja sababu tatu za kutoshiriki chaguzi hizo ikiwamo ya kutoandikishwa kwa wapigakura wapya tangu 2015, hujuma, kutumika kwa nguvu ya vyombo vya dola na kutishwa kwa wapigakura.

“Hatuwezi kushiriki chaguzi hizo kwa sababu kuna watu tayari wamechukua fomu Liwale wakidai wao ni Chadema, wakienda walioteuliwa na chama hawatapewa fomu,” alidai Mbowe.

Wakizungumza na Mwananchi jana, viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na wanazuoni walitoa maoni yao juu ya uamuzi wa chama hicho kutoshiriki uchaguzi mdogo wa Jimbo la Liwale mkoani Lindi na kata 37 utakaofanyika Oktoba 13.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema uamuzi wa Chadema kususia chaguzi hizo huenda ukawa si sahihi na badala yake, alishauri chama hicho kiendelee kushiriki ili kushinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya Katiba.

Alisema ni muhimu kushughulikia kiini cha matatizo na dosari zinazojitokeza kwenye chaguzi za marudio kwa kuendelea kushinikiza kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.

“Faida ya kushiriki ni moja tu, wanapata nafasi ya kuzungumza na wananchi na kurekodi matatizo. Tume haijabadilika na haitabadilika hadi 2020, ndiyo mfumo uliopo. Kwa hiyo kususia hakusaidii.”

Hata hivyo, alisema suala hilo la kuishinikiza Serikali litabaki kuwa gumu kutekelezeka endapo vyama vya upinzani havitaunganisha nguvu na kuwa na uamuzi wa pamoja.

“Wangeendelea kushiriki, ili haya matatizo yawekwe wazi kusudi kusiwe na chama kimoja kinachofanya uamuzi,” alisema Profesa Mpangala.

Alisema vyama vya upinzani vina uwezo wa kuwashirikisha wadau wengine zikiwamo asasi za kiraia, wasomi na viongozi wa dini ili kudai mabadiliko na si kususia uchaguzi.

“Kinachotakiwa sasa hivi ni mjadala wa kitaifa ili kudai marekebisho hasa ya misingi ya demokrasia na utawala bora,” alisema.

Kauli hiyo inakuja huku tayari NEC ikiwa imeeleza kuwa kila chama kina haki ya kushiriki uchaguzi huo na haiwezi kulazimisha kama chama kimesema kinaendelea kufanya tathmini ya uchaguzi ujao.

Hata hivyo, Hoja ya Profesa Mpangala ilipingwa na msomi mwingine, Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye alisema uamuzi huo wa Chadema ni sahihi huku akionyesha wasiwasi wake wa nchi kuelekea kwenye mfumo wa chama kimoja.

“Kwa nini waendelee kuingia kwenye uchaguzi ambao wanajua hawatashinda? Nafikiri uamuzi wao ni sahihi, waache hadi hapo Katiba itakapobadilisha tume ya uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi,” alisema.

“Labda turudi kwenye chama kimoja na upinzani uwe ndani ya CCM kama tulivyokuwa awali. Tulikuwa na Tanu na ndani yake kulikuwa na upinzani,” alisema.

Kuhusu hoja ya Chadema ya kukihuisha chama, Profesa Shumbusho alisema hali haiwezi kubadilika hadi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020.

Vyama vingine vya upinzani

Akizungumzia msimamo wa chama chake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kilichoamuliwa na Chadema ni sahihi kwa masilahi mapana ya Taifa.

“Kwa sababu siku hizi hakuna uchaguzi, mnashiriki uchaguzi gani? hakuna uchaguzi unaofanyika,” alidai Mbatia.

Alitaja mambo mawili, moja ni vyombo vya dola kushabikia siasa na wateule wa Rais kuwa makada wa CCM hasa kwenye Tume ya Uchaguzi.

“Haya waliyofanya Chadema yasionekane ya Chadema, hiki ni kiashiria cha watu kutoridhika, ukiona chama kikuu cha upinzani kama Chadema kinachukua hatua hiyo, ujue kuna viashiria vingi wanaelekea kukata tamaa,” alisema Mbatia.

Katibu Mkuu wa NLD, Tozy Matwanga aliunga mkono msimamo huo akisema “Huwezi kufanya uchaguzi ambao huwezi kushinda.”

Alisema NEC na vyombo vya dola vinavuruga uchaguzi hali inayojenga hofu kwa wananchi kushiriki.

Hata hivyo, alisema upinzani hauwezi kufa na badala yake unazidi kuimarika kwa kuwa upinzani si viongozi, bali ni wanachama.

“Hata sisi hatutashiriki kwa sababu hata tukishiriki hatuwezi kushinda,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Joran Bashange alisema; “Nchi hii haijawai kuwa na uchaguzi kila mwezi... kwa hiyo kwa upande mwingine kushiriki ni kama tunahalalisha haramu.”

Alisema vyama vya upinzani vinatakiwa kukaa pamoja na kuweka mikakati ili kuona namna bora ya kushiriki chaguzi zijazo kwa masilahi ya wananchi.

Maoni ya wananchi

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa jijini Mbeya wametoa maoni tofauti kuhusu uamuzi huo wa Chadema.

Mkazi wa Soko Matola, Modest Shiyo alisema ni sahihi kwa Chadema kujitoa kwa madai kuwa hata wakishiriki hawawezi kushinda. “Naamini jitihada za Rais kutatua kero za wananchi ni sababu kubwa kwa Chadema kukosa hoja na kuamua kujiondoa kwenye uchaguzi huo.”

Hata hivyo alisema hafikirii kwamba kujiondoa kwa Chadema kutasaidia kumaliza matatizo wanayolalamikia.

Mkazi wa Makunguru, Daudi Mwalulesa, alisema ni sahihi kwa sababu kumekuwa na vitendo vya ukiukwaji wa demokrasia katika kila uchaguzi. “Uamuzi huu ni sahihi sana, ni boara CCM iendelee kushinda ikiwa peke yake.”

Samweli Mdolo mkazi wa Nonde alisema haoni kama ni sahihi Chadema kujiondoa kwa sababu wanajenga mwanya wa kusahauliwa na wananchi.

UVCCM wazungumza

Katibu wa Idara ya Hamasa na Chipukizi ya UVCCM, Hassan Bomboka alisema Mbowe atafute sababu nyingine za kujitoa kwenye uchaguzi badala ya kutafuta huruma kwa wananchi kwa kutamka mambo yasiyokuwa na ushahidi.

Alisema hoja kumi na moja alizozitoa hazina mashiko.

“Mbowe anampangia mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama lini aende kuzungumza na watu wake wa vyombo vya ulinzi na usalama wa mkoa na wazungumze nini.

“Nilidhani kungekuwa na mifano ni wapi Polisi walimuwekea raia silaha iwe Ukonga au Monduli au kwenye kata na kumlazimisha kumpigia kura mgombea wa CCM hapo tungemuelewa, lakini hakuna pingamizi wala malalamiko ya Polisi kuvunja sheria aliyoyaripoti kwenye vyombo vya dola,” alisema.

Nyongeza na Kalunde Jamal Dar, Yonathan Kossam, Mbeya