Uamuzi wa Ndalichako una msukomo wa kisiasa?

Muktasari:

Profesa Ndalichako amepiga marufuku kusoma masomo ya shahada bila kupitia kidato cha sita na kwamba marufuku hiyo itaanza rasmi katika mwaka ujao wa masomo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametoa uamuzi mpya kuhusu wanafunzi wanaostahiki kujiunga vyuo vikuu nchini.

Profesa Ndalichako amepiga marufuku kusoma masomo ya shahada bila kupitia kidato cha sita na kwamba marufuku hiyo itaanza rasmi katika mwaka ujao wa masomo.

Akizungumza katika maonyesho ya vyuo vikuu na taasisi za elimu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Ndalichako alisema mfumo wa elimu huria umechangia kuzalisha wasomi butu kwa kupokea wanafunzi dhaifu kitaaluma.

Ndalichako alisema wanafunzi wanaofeli kidato cha nne na kwenda kusomea cheti (certificate) na baadaye diploma ili wajiunge vyuo vikuu hawataruhusiwa kujiunga na masomo ya shahada kama hawajarudia (reseat) masomo yao na kupata alama za kwenda kidato cha tano na wafanye mitihani ya kidato cha sita na kufaulu ndipo wajiunge vyuo vikuu.

Katika utaratibu huo, wanafunzi wa kidato cha nne watakaoruhusiwa kusoma shahada bila kupita kidato cha tano na sita ni wale waliofaulu kidato cha nne na wakachaguliwa kwenda kusoma katika vyuo vya ufundi daraja la kati.

Hata hivyo, wale wanaokosa sifa yaani ‘credit’ za kuendelea na kidato cha tano na kuamua kwenda kusomea cheti mwisho wao utakuwa astashahada (diploma) na diploma zao hazitaruhusiwa kutumika kama sifa ya kujiunga chuo kikuu hadi watakapofanya mitihani ya kidato cha nne na kufaulu.

Kuhusu kozi za msingi kwa wanafunzi wa kidato cha sita walioshindwa kupata sifa za kusoma chuo kikuu, Ndalichako alisema kozi hiyo haimuongezei mtu sifa za kujiunga na chuo kikuu.

“Kama mtu amemaliza kidato cha sita akashindwa kufikisha nukta (points) za kujiunga chuo kikuu, asidahiliwe kwa kusoma foundatiom course yaani kozi ya msingi.

“Anapaswa kurudia mtihani wa kidato cha sita kwa sababu baraza la mitihani linatoa fursa ya kurudia mara nyingi iwezekanavyo. Foundation course haimuongezei mtu sifa kama hana sifa zinazotakiwa kitaaluma,” alisisitiza Ndalichako.

 

Watumishi waliosoma ‘bila sifa’ kupoteza ajira

Jambo jingine lililoshtua zaidi ni pale waziri alipotoa kauli kwamba watu wote walioajiriwa lakini walisoma vyuo vikuu pasipo kuwa na sifa kuondolewa kazini.

“Kama wewe ni mfanyakazi uliyesoma moja ya vyuo vikuu ukafaulu lakini hukuwa na sifa ya kujiunga na chuo hicho tutakunyofoa huko huko kwenye ajira yako,” alieleza Waziri Ndalichako.

Waziri aliweka wazi kwamba hivi sasa bado wanaendelea na zoezi la kuwatafuta wanafunzi wanaonufaika na mkopo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) lakini hawakuwa na sifa ya kujiunga na vyuo vikuu.

“Tukimaliza wanafunzi hawa wanaopata mikopo ya Serikali, tunahamia kwa wengine wasio na mikopo na baadaye kwa wafanyakazi. Hata kama hunufaiki na mkopo na huna sifa hauko salama,” alisema Ndalchako.

 

Hebu tujadili

Matamshi ya waziri huyu mwenye dhamana ya elimu na ufundi na hivyo mustakbali wa Taifa kwa kuwa taifa lolote lile bila elimu na ufundi halina mustakbali, yamezusha mijadala mikali nchini.

Ukiyatafakari maneno ya Profesa Ndalichako kwa juu juu unaweza kuona ni uamuzi mzuri unaolenga kuboresha elimu yetu kwa sababu utachochea usomaji wa wanafunzi kwa bidii kwa kujua hakuna tena njia ya mkato.

Hata hivyo, ndani ya uamuzi huo kuna janga linalolisubiri taifa siku za usoni. Kwanza, waathirika wakubwa wa uamuzi huo ni wale wanafunzi wa watoto wa walala hoi ambao husoma katika shule za kata.

Shule hizi ambazo zimetelekezwa na Serikali kiasi cha kupewa jina shule za ‘Yebo Yebo’ au ‘St. Kayumba’ ndizo zenye idadi kubwa ya wanafunzi ambao kwa kukosa mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia hujikuta wakishindwa kujiunga na kidato cha tano.

Isitoshe, hata Serikali yenyewe imekiri kwamba haina shule za kidato cha tano na sita za kutosha kiasi kwamba wanafunzi wengi hukosa nafasi ya kuendelea na masomo yao kidato cha tano.

Hata wale waliofaulu na kujiunga na kidato cha tano Serikali huwaacha kwa madai kwamba wana umri mkubwa. Juni 25, mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alitangaza majina ya wanafunzi 24,258 waliokosa nafasi kujiunga na kidato cha tano.

Kwa mujibu wa Simbachawene, idadi hiyo ni sawa na asilimia 27.2 ya waliofaulu wakiwamo wasichana 6,789 na wavulana 17,739 wamekosa nafasi ya kujiunga na shule za sekondari kidato cha tano na sita na vyuo vya ufundi vinavyomilikiwa na Serikali.

Alitaja sababu za wanafunzi hao waliofanya mitihani ya kumaliza elimu ya kidato cha nne mwishoni mwa mwaka jana kukosa nafasi hizo kuwa ni kutokana na ufinyu wa nafasi za shule na vyuo hivyo.

Pia, aliitaja sababu nyingine kuwa ni kutimiza umri wa zaidi ya miaka 25 na kusababisha kutokuwa na sifa za kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano.

Ukiufahamu ukweli huu na kisha kuitafakari kauli ya waziri Ndalichako aliposema kwamba aliyefeli anapaswa kurudia mtihani wa kidato cha sita kwa sababu baraza la mitihani linatoa fursa ya kurudia mara nyingi iwezekanavyo, utaona mkanganyiko mkubwa.

Waziri anawataka wanafunzi kurudiarudia mara nyingi iwezekanavyo na katika kufanya hivyo ni wazi ndiyo maana wanafunzi hao wanafikia umri wa miaka zaidi ya 25.

Halafu wakishazidi umri huo Serikali inawanyima nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano. Utagundua kwamba katika suala la elimu, uamuzi uliokuwa ukitolewa tangu Serikali zilizopita umefanyika kisiasa, kwa kukurupuka, bila kufanya utafiti na bila kuwashirikisha wadau wa elimu nchini.

Niliongea na mmoja wa viongozi wa wamliki wa shule na vyuo visivyo vya Serikali nchini yaani Tamongsco kutaka kujua kwa nini mawaziri wa elimu nchini kila ajaye huingia na mabadiliko anayoyataka?

Akajibu kwamba tatizo ni kutokutekelezwa kwa Sheria ya Elimu namba 5 ya mwaka 1978. “Unajua ndugu yangu sheria ya elimu inatamka wazi kuwa waziri anapaswa kuunda baraza la ushauri kumshauri katika masuala kama haya, lakini mawaziri wote walioshika nafasi hiyo hawajali kutekeleza matakwa haya ya kisheria ipasavyo,” alisema kiongozi huyo.

Ni wazi jambo hili la kuzuia wanafunzi waliopitia vyuo na kufikia diploma lilihitaji ushirikishwaji wa wadau wa elimu kwa sababu utekelezaji wake utapeleka kilio kwa wanafunzi wengi.

Huko nyuma aliyekuwa waziri wa elimu, Joseph Mungai aliwahi kufumua mitalaa ya elimu na kufuta masomo huku akiunganisha mengine.

Alipokuja waziri Dk Shukuru Kawambwa naye akaja na yake yakiwamo ufaulu kwa GPA ambao kimsingi ulikuwa uamuzi wa kisiasa kuficha aibu ya kufeli kwa wanafunzi na kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.

Akishangaa kauli ya Waziri Ndalichako, mmoja wa wadau wa elimu aliyewahi kuwa mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema: “Nilikuwa ninaongoza kitengo cha shahada ya jioni. Idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa wanatoka kwenye diploma na mitihani ya mature entry. Na wapo ambao walifaulu na kuendelea na shahada ya pili na wanafanya kazi vizuri tu.”

Mhadhiri Tawakkal Hussein wa Chuo cha Waislamu Morogoro (MUM) alisema :“Mpango huu unapaswa kupingwa kwa nguvu zote kwa kuwa sababu alizotoa waziri si za kweli.

“Ninaye jamaa yangu ambaye amepitia utaratibu huo baada ya kumaliza shule za kata na kukosa matokeo mazuri ya kumfanya aingie kidato cha tano. Amehitimu digrii yake na ufaulu wa daraja la kwanza,” alisema.

Mdau mwingine alimtaka Waziri Ndalichako kuachana na mpango huu kwa sababu kama mtu anaweza kusoma digrii yake na akafaulu, haina maana kumzuia asisome kwa kuwa ameingia chuoni akiwa na diploma.

“Hivi tunachotaka ni punda au mlio wa punda? Hivi waziri hajui kwamba hata bilionea Bill Gates aliyesifika kwa ugunduzi wa kompyuta hakufikia hata hiyo diploma aliishia grade six?” alihoji mdau huyo.

Wadau wengi wameitaka Serikali kufungua mjadala wa wazi kuhusu hatua hiyo ya Ndalichako huku wakimhimiza kuunda haraka baraza la ushauri la elimu kumshauri waziri kuhusu mambo kama haya badala ya kila siku kuibuka na kauli za kiimla.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na [email protected]