Ubalozi wa Vatican kuhamia Dodoma

Muktasari:

Waziri Mkuu awaagiza CDA watafute kampuni zenye uwezo wa kupima viwanja haraka

Dodoma. Wakati Serikali ikiendelea kuhamia mjini hapa, Askofu Mkuu wa Jimbo la Katoliki Dodoma, Beatus Kinyaiya amepeleka ombi kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kupewa eneo la kujenga ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), ubalozi wa Vatican, makazi ya balozi wa Baba Mtakatifu, Papa Francis 16 na viongozi wakuu.

Askofu Kinyaiya alisema walipowasilisha maombi yao Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), waliahidiwa kupatiwa eneo la makazi lakini wanahitaji la ofisi.

Akiwa ameongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC),Peter Maduki, Askofu Kinyaiya alimtembelea Waziri Mkuu ofisini kwake Mtaa wa Railway, mjini Dodoma jana.

Majaliwa alisema amefurahishwa na uamuzi wa CCT kutafuta viwanja Dodoma ili wajenge ofisi pamoja na makazi ya viongozi wao wakuu.

Alisema wiki tatu zilizopita alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa CDA atafute kampuni zenye uwezo wa kupima viwanja kwa haraka.

“Hii itatusaidia kutambua kama tuna eneo la ukubwa gani na mahitaji halisi ni yapi na nani akija apewe eneo lipi kulingana na mahitaji yake,” alisema.

Aliyashukuru makanisa kwa huduma za kijamii zitolewazo katika sekta za elimu, afya na kilimo kama ambavyo ameshuhudia katika baadhi ya maeneo alikopita nchini.

Alikubali ombi lao la kuwa na kikao cha pamoja baina ya watendaji wa Serikali na makanisa kitakachojadili namna ya kuimarisha ubia katika utoaji wa huduma za kijamii hususan za afya na elimu. “Kikao hiki kitalenga kufanya mapitio ya huduma zinazotolewa baina ya Serikali na makanisa lakini kitatusaidia kupata mrejesho wa mambo yanayofanyika kwenye hospitali na shule mnazomiliki katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema Majaliwa.