Ubinafsi wa viongozi wakwamisha ujenzi sokoni

 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.

Muktasari:

Makalla alieleza sababu hiyo juzi kwenye mkutano wa hadhara na wafanyabiashara hao uliofanyika katika soko hilo.


Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ameeleza sababu za kusimamisha ujenzi wa vyoo na vibanda vya wafanyabiashara 459 katika Soko la Uhindini mkoani humo kuwa ni kutokana na baadhi ya watumishi na madiwani kugawana maeneo hayo.

Makalla alieleza sababu hiyo juzi kwenye mkutano wa hadhara na wafanyabiashara hao uliofanyika katika soko hilo.

Alitoa muda wa siku 21 ujenzi wa vibanda vipya uanze chini ya usimamizi wa halmashauri ya jiji.

Makalla alisema anasikitishwa na baadhi ya watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kutokuwa na hofu ya Mungu kwa kujiingiza kinyemela kujigawia maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya biashara huku wahusika wakiachwa.

“Ndugu zangu mimi nimekuja Mbeya nimeaminiwa na Rais, sasa kitendo kisicho cha kiungwana kwa watumishi tena madiwani kujigawia maeneo na ninapozungumza hapa nina majina yao,” alisema.

Makalla alisema alikuwa na nia njema na wafanyabiashara kurudi katika eneo hilo, lakini alishangazwa na hatua ya kuanza ujenzi huo kimyakimya ambao ungewanufaisha wachache.

Pia, Makalla alifuta ujenzi wa choo na vibanda vinane vilivyojengwa kwa ajili ya mfano na kuagiza jiji kuanza upya kuchora ramani ya soko hilo.

Awali, wafanyabiashara hao walisema waliounguliwa na vibanda soko lilipopata ajali ya moto mwaka 2010 walikuwa 140, lakini sasa kuna majina zaidi ya 300.

Mfanyabiashara, Sekela Mwakabungu alisema ni jambo jema kwa suala hilo kufikishwa kwa mkuu wa mkoa kwa kuwa hata kamati ya wafanyabiashara iliyoundwa wengi wao siyo wahusika.

‘’Huu uongozi wa jiji haujatenda haki na hauna huruma na wafanyabiashara kwa kuwa hapa tayari wafanyabiashara wengi ambao hawana fedha wangekosa vibanda,’’ alisema Mwakabungu.

Mfanyabiashara mwingine, Brown Mwandambo alisema hawana imani na kamati iliyoundwa kuhakiki majina na kwamba haijatenda haki kwa kuwa imetoa kipaumbele kwa watu wasiohusika.

Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Laynas Sanya alisema alishangazwa na ujenzi kuendelea bila kushirikishwa wakati ramani ya soko alikuwa nayo yeye ofisini kwake.