Uboreshaji upatikanaji mikopo waipaisha Tanzania

Muktasari:

Ripoti mpya ya mazingira ya biashara ya mwaka 2017 iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) jana, inaonyesha Tanzania imekuwa nchi ya 132 kutoka 139 mwaka jana duniani na ya nne ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Rwanda, Kenya na Uganda.

Dar es Salaam. Uboreshaji wa upatikanaji mikopo unaosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umeipandisha nchi kwa nafasi saba katika mazingira ya biashara duniani, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika miaka mitano iliyopita.

Ripoti mpya ya mazingira ya biashara ya mwaka 2017 iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) jana, inaonyesha Tanzania imekuwa nchi ya 132 kutoka 139 mwaka jana duniani na ya nne ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Rwanda, Kenya na Uganda.

Meneja Mradi wa Ufanyaji Biashara wa WB, Rita Ramalho alisema Tanzania ilipanua wigo wa upatikanaji wa taarifa za mikopo zinazohusu kampuni, mashirika na watu binafsi ambazo ni muhimu kwa taasisi za fedha katika uamuzi wa utoaji na udhibiti wa mikopo.