Ubungo Plaza wawatimua Blue Pearl

Mlinzi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, akifunga geti la iliyokuwa Hotel ya Blue Pearl ambayo imefungwa kwa madai ya kutolipa kodi ya pango jijini Dar es Salam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Awali, uongozi wa Ubungo Plaza ulifungua kesi Mahakama ya Ardhi

Dar es Salaam. Uongozi wa Ubungo Plaza Limited umesema umeamua kumfungia mpangaji wake, Hoteli ya Blue Pearl kwa madai kuwa aliacha kulipa kodi ya pango tangu Mei, 2014.

Hata hivyo, uongozi wa hoteli hiyo uliokuwa ukishughulikia kuwahamisha wateja wake jana, haukuwa tayari kuzungumzia madai hayo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ubungo Plaza, Harun Mgude alisema jana kuwa uamuzi wa kuifungia hoteli hiyo umefikiwa baada ya kushinda kesi Mahakama ya Ardhi.

“Blue Pearl amekuwa mpangaji wetu tangu mwaka 2006 na mkataba wake ulikuwa wa miaka 15 ambao ungeisha 2021. Alikuwa akilipa vizuri lakini tangu Mei, 2014 aliacha kulipa,” alidai Mgude.

Alifafanua kuwa kutokana na hilo walikwenda kufungua kesi Mahakama ya Ardhi na Blue Pearl wameshindwa, hivyo walitakiwa kulipa au kutoka ndani ya jengo.

“Kama mnakumbuka tuliwahi kumtoa na akarudi kwa amri ya Mahakama ili kupisha kesi kuendelea, lakini Novemba 3, 2017 kesi iliisha na ameshindwa na kutakiwa kulipa deni la Sh5.7 bilioni,” alidai.

Alisema kuwa uongozi wa Blue Pearl umeomba kufanya kikao Jumatatu ili kujadili namna ya kulipa deni hilo.

“Baadhi ya wateja wamehamishiwa hoteli nyingine sijui ni wapi. Ila ieleweke kuwa robo tatu ya mali zilizokuwamo Blue Pearl ni za Ubungo Plaza Limited kama vile furniture (samani) na vitu vingine,” alisema Mgude. Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, Scholastika Kevela alisema, “Tunafunga (hoteli) na kukabidhi kwa mmiliki na shughuli hapa hazitaendelea tena hadi awe amelipa kodi.”

Mmoja wa wateja, Masoud Masoud akiwa na familia yake alisema, “Nimetoa hela nyingi na ilikuwa nikae kama wiki mbili, nimeingia jana, huu ni usumbufu.”