Uchumi wa makaratasi wakua, mifukoni taabani

Gavana wa Benki  Kuu (BoT),Profesa Benno Ndulu

Muktasari:

Pato hilo limeongezeka kwa asilimia moja, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Dar es Salaam. Kukua kwa Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 6.7 katika nusu ya kwanza ya mwaka kumegonga vichwa vya wasomi wakitofautiana kuhusu maana yake kwa mwananchi wa kawaida.

Pato hilo limeongezeka kwa asilimia moja, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Januari mpaka Juni mwaka jana, GDP ilikua kwa asilimia 5.7 na hali inayoonyesha kuimarika kwa pato hilo mwaka huu.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Dianna Mwiru alisema kasi hiyo haishangazi kwani imeshawahi kuwapo: “Hizi ni namba tu. Itakuwa na maana zaidi iwapo Watanzania wanaoishi kwenye mstari wa umaskini wangepungua.”

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Mutahyoba Baisi alisema kushuka kwa mchango wa sekta ya ujenzi kumetokana na uamuzi wa Serikali kubana matumizi na kudhibiti rushwa miongoni mwa watendaji wake.