#TanzaniaYaViwanda : Uchumi wa viwanda una historia ndefu Tanzania…

Muktasari:

  • Wakati tukijiandaa kwa tukio hilo la kihistoria, tunakuletea mfululizo wa makala zinazobainisha fursa na kubainisha changamoto zilizopo. Leo tunakuletea historia yenye sera kuhusu kufanikisha ndoto hiyo. Endelea...

Utekelezaji wa dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2025 unatarajiwa kuipandisha hadhi Tanzania kuwa ya kipato cha kati.

Lengo hilo litatimia kutokana na misingi imara iliyowekwa na uongozi imara wa awamu zilizopita ambao sasa Serikali inaendeleza juhudi zilizofanywa na viongozi waliopita.

Historia ya viwanda nchini inaanza tangu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere (1962-85) na, Azimio la Arusha na sera ya chama cha Tanu ya ujamaa na kujitegemea ya Februari 5, 1967.

Ikiwa ni miaka michache tangu Tanzania ilipopata uhuru kutoka kwa mkoloni, azimio hilo lilikusudia kujenga uchumi imara utakaokidhi mahitaji ya ndani ya Serikali na wananchi pia.

Pamoja na mambo mengine, sera hiyo ililenga kujenga viwanda hasa vitakavyozalisha bidhaa muhimu zinazohitajika kwa matumizi ya kila siku.

Serikali ilikusudia kuwa na viwanda vitakavyochakata malighafi zote zinazozalishwa nchini na mkazo ukaelekezwa zaidi sekta ya kilimo na rasilimali nyingine za maliasili.

Kutokana na ukubwa wa sekta ya kilimo kinachoajiri asilimia kubwa ya Watanzania, sera ya chama na malengo ya azimio yalikusudia kuongeza thamani ya mazao kupata bidhaa maridhawa kwa mahitaji ya soko.

Baada ya kuongeza thamani, bidhaa za viwandani huuzwa kwa bei kubwa kidogo hivyo kuimarisha kipato cha wakulima, kuongeza mzunguko wa fedha na kukuza mapato ya Serikali.

Mapinduzi ya viwanda

Kwenye uzalishaji viwandani, mashine na mitambo hutumika zaidi badala ya juhudi za nguvukazi ili kupata bidhaa nyingi zaidi kwa muda mfupi.

Utafiti unabainisha mapinduzi ya viwanda yamechangia mgawanyo wa kazi, matumizi ya teknolojia ya kisasa na ubunifu wa changamoto zinazojitokeza ndani na nje ya uzalishaji tofauti na kutegemea hali ya mazingira ambayo yapo nje ya uwezo wa mwanadamu.

Kulingana na muda, viwanda vinakusudiwa kuchangia kukuza uchumi hivyo maendeleo katika nyanja tofauti za kijamii.

Baadhi yetu, ama tumesikia au tunafahamu historia ya mapinduzi ya viwanda yaliyotokea nchini Uingereza jinsi yalivyobadili uchumi wa nchi hiyo na dunia kwa ujumla.

Mapinduzi hayo ya Uingereza yalifanyika kati ya mwaka 1760 hadi 1840 na kuacha mabadiliko makubwa ya jamii za Waingereza na kwingineko ikiwamo Tanzania.

Baada ya utekelezaji wa Azimio la Arusha kwa miaka kadhaa tangu lilipoanzishwa likizuia viongozi wa umma kufanya biashara, lilikufa mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Kufa kwa Azimio la Arusha kulileta Azimio la Zanzibar lililoanzishwa Februari 1991 ambalo lilifanya maboresho ya azimio lililotangulia kwa kuwaruhusu viongozi kuingia kwenye biashara.

Kwa mabadiliko hayo sasa, viongozi wa umma waliruhusiwa kuongeza vyanzo vyao vya mapato wakiruhusiwa kupokea mshahara zaidi ya mmoja, kumiliki hisa za kampuni na mashirika au kumiliki majengo ya kupangisha.

Vilevile, waliruhusiwa kuwa wakurugenzi wa mashirika hata kampuni binafsi mambo yaliyoharamishwa na Azimio la Arusha.

Kwenye azimio hilo jipya, viongozi wa umma waliruhusiwa kujenga au kuanzisha viwanda, kusaidia kuhamasisha sekta hiyo muhimu kwa mahitaji ya wananchi nchini.

Mkakati uliopo

Baada ya Rais John Magufuli kuchaguliwa na kuapishwa kuiongoza Tanzania, mwishoni mwa mwaka 2015, amekuwa akihimiza ujenzi wa viwanda nchini.

Lengo lililopo ni kuhakikisha sekta hiyo inachangia asilimia 40 kwenye pato la Taifa (GDP) ifikapo mwaka 2025 na kuongeza ajira hasa kwa vijana na wanawake.

Dk Magufuli anaamini, na ameshawahi kusema, viwanda ndio kipaumbele cha Serikali bila kujali changamoto zitakazojitokeza.

Taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha mpaka mwishoni mwa mwaka 2016, Tanzania illikuwa na viwanda 49,243 vingi (asilimia 98.4) vikiwa ni vidogo sana vinavyoongeza thamani ya malighafi zilizopo nchini.

Jambo la kuvutia ni kwamba, viwanda vikubwa viliongezeka kutoka 729 vilivyokuwapo mwaka 2008 mpaka 1,322 mwaka 2016 kwenye uunganishaji magari, chuma, uzalishaji saruji na kusindika mazao ya kilimo.