Uchunguzi kesi ya vigogo wa uthamini madini haujakamilika

Muktasari:

Washtakiwa Archard Kalugendo na Edward Rweyemamu wanakabiliwa na shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4 bilioni wakidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wawili wa uthamini wa madini ya almasi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 8, 2018 na wakili wa Serikali, Saada Mohammed mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri, kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Mohammed amedai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba jalada la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kwamba kuna utaratibu anaumalizia.

Baada ya wakili huyo kueleza hayo, Hakimu Mashauri aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 22 mwaka huu na kuwaeleza washtakiwa siku hiyo watasikiliza maendeleo ya kesi yao.

Washtakiwa  wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania (Tansort), Archard Kalugendo na mthamini almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu ambao ni waajiriwa wa Wizara ya Nishati na Madini.

Kalugendo na Rweyemamu wanasota mahabusu kutokana na DPP kuzuia dhamana zao na wanakabiliwa na  kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh 2.4 bilioni.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya Sh 2.4 bilioni ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

Washtakiwa hao wanadaiwa kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathaminishaji wa almasi wa serikali na waajiriwa wa wizara hiyo waliisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 1.1 milioni ambazo ni sawa na sh 2.4 bilioni.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.