Udom waanza kufanyia kazi hoja ya Mkapa

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa 

Muktasari:

Ingawa sera na sheria zimezungumzia huduma kwa walemavu, lakini hazijaweza kutekelezwa vizuri kama inavyotakiwa


Dodoma. Siku chache baada ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kutaka mdahalo wa uwazi kujadili elimu, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimekutana na makundi ya jamii kujadili elimu kwa watoto wenye ulemavu na kubaini upungufu katika utekelezaji wa sheria na sera.

Akizungumza leo Machi 24, 2018, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu cha Udom, Enedy Mlaki amesema mkutano huo unaojumuisha makundi mbalimbali ya kijamii unalenga katika kusikia mawazo mbalimbali ya wadau wa elimu.

Amesema lengo ni kupata mawazo ambayo yatajenga mfumo mzima wa elimu jumuishi na hivyo kutowaacha nyuma watoto wenye ulemavu.

“Na kama mlivyosikia mwaka jana kuna shule moja kule Njombe wanafunzi karibu wote walifeli na sisi tukasema kama Chuo Kikuu cha Dodoma ambao tunaongoza kwa kutoa elimu bora tufanye kitu,” amesema Mlaki.

Amesema wameamua kuchambua sera za elimu zinazohusu wanafunzi ambao wana mahitaji maalumu ili kupata mawazo ya makundi mengine ya jamii juu ya maeneo hayo.

Mkuu wa Idara ya Saikolojia wa chuo hicho, Dk January Basela amesema Tanzania ina sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 na sheria inayoongoza huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2010.

Amesema sera iliyopo haijazungumza kwa upana juu ya majukumu ya kila mmoja nchini katika kuhakikisha utekelezaji wa sheria na sera zilizotungwa.

“Lakini sera haifafanui ni kwa namna gani watu wenye ulemavu wanapata haki zao na huduma mbalimbali kama matibabu,” amesema.

Amesema ingawa sera na sheria zimezungumzia huduma kwa walemavu, lakini hazijatekelezwa vizuri kama inavyotakiwa.

“Kuna sheria zipo, kuna sera zipo lakini bado lakini utekelezaji wake ni mgumu hazijaweza kutekelezeka kwa kina inavyotakiwa,” amesema.

Ameshauri miundombinu ya elimu iwe rafiki ili kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kuwawezesha kupata huduma na elimu.