Ufaransa yajitosa kuibeba Tanzania kufikia uchumi wa kati

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier akizungunmza wakati wa mahojiano maalum na waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Balozi huyo alisema ushirikiano baina ya mataifa haya mawili umedumu kwa muda mrefu na nia iliyopo kwa sasa ni kuimarisha diplomasia ya kiuchumi.

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier amesema Serikali yao itaisaidia Tanzania kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo ili kuirahisishia kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.

Kwa miaka michache iliyobaki kabla ya kufika mwaka wa makusudio ya kukuza uchumi huo, Clavier amesema Ufaransa itaongeza zaidi ya maradufu ufadhili iliokuwa inautoa awali. “Kwa muongo mmoja uliopita tulikuwa tunaisaidia Tanzania wastani wa Euro 50 milioni kila mwaka. Kwa miaka mitano ijayo tutaongeza fedha hizo mpaka wastani wa Euro 100 milioni kuiwezesha kuwa ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Clavier, juzi.

Balozi huyo alisema ushirikiano baina ya mataifa haya mawili umedumu kwa muda mrefu na nia iliyopo kwa sasa ni kuimarisha diplomasia ya kiuchumi.

Alisema Ufaransa itatoa ushirikiano unaohitaji kufanikisha miradi ya kipaumbele ambayo Serikali itajiwekea kwa manufaa ya wananchi.

Balozi huyo alisema hayo juzi usiku kwenye hafla ya kusherehekea miaka 10 ya uwepo wa Shirika la Maendeleo Ufaransa (AFD) nchini, ambalo kwa kipindi hicho limechangia zaidi ya Sh1.4 trilioni kwenye sekta za maji, nishati na usafirishaji.

Kaimu katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shaaban aliishukuru Ufaransa na kuliomba shirika hilo kuongeza ushawishi wake nchini.

“Tunawakaribisha mfungue ofisi za wakala kamili nchini, lakini nawaomba nendeni Zanzibar pia. Msikae Bara pekee, Tanzania ni kubwa,” alisema Amina.

Tangu mwaka 2008 ilipofungua ofisi zake nchini, AFD imekuwa ikitoa mikopo ya riba nafuu kusaidia kufanikisha miradi ya maji na usafi wa mazingira, nishati na usafirishaji.

Ofisa mtendaji mkuu wa AFD, Remy Rioux alisema anaamini sekta hizo ni muhimu na zina mchango mkubwa kwenye utekelezaji wa dhamira ya kuwa na uchumi wa viwanda. “Tutaendelea kujikita kwenye sekta hizo kwenye miradi ya umma. Lipo dirisha la kuiwezesha sekta binafsi pia,” alisema Rioux.

Ofisa mtendaji mkuu huyo yupo nchini kwa ziara ya siku mbili iliyoanza juzi mpaka jana, akikutana na wadau muhimu hasa viongozi wa Serikali.

Pamoja na mambo mengine, alizindua ofisi ya wakala wa AFD ambao awali huduma zake zilikuwa zinapatikana kutoka Kenya.